Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

WAZIRI MKUU MHE. MAJALIWA ATOA WITO VYA MADHEHEBU YA DINI KUHIMIZA HIFADHI YA MAZINGIRA

30 Nov, 2022
WAZIRI MKUU MHE. MAJALIWA ATOA WITO VYA MADHEHEBU YA DINI KUHIMIZA HIFADHI YA MAZINGIRA
SERIKALI imetoa wito kwa viongozi wa dini nchini kuhamasisha utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi yanayotishia mustakabari wa Taifa kutokana na madhara yanayojitokeza dhahiri ikiwemo ukame na upungufu wa mvua.
 
Wito huo Umetolewa mjini Arusha na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati wa Ibada maalumu ya kustaafu kwa Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Bw. Brighton Kilewa na kuingizwa kazini Katibu Mkuu mpya wa Kanisa hilo Mhandisi Robert Kitundu, ibada iliyofanyika katika Usharika wa Ngarenarok, Dayosisi ya Kaskazini Kati.
 
Mheshimiwa Majaliwa amepongeza hatua zinazochukuliwa na Kanisa hilo pamoja na makanisa mengine kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira na kuomba agenda hiyo ichukuliwe kwa uzito wake na madhehebu yote ya dini pamoja na wananchi wote kwa ujumla ili kudhibiti uharibifu huo wa mazingira.
 
“Nimefurahi kusikia kanisa linaunga mkono matumizi endelevu ya maliasili tulizopewa na Mungu, vilevile nimefurahi kusikia Kanisa linatambua wajibu wa kutunza mazingira, kama alivyosema Baba Askofu (Dkt. Shoo), hali ya utunzaji wa mazingira hapa nchini si mzuri, vyanzo vya maji ikiwemo mito vimekauka” alifafanua Dkt. Nchemba kwa niaba ya Waziri Mkuu.
 
“Viongozi wa dini katika mahubiri yenu wekeni msisitizo katika masuala ya utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji miti na matumizi ya nishati mbadala wa kuni na mkaa, Nitoe wito kwenu viongozi wa dini endeleeni kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira” aliongeza Dkt. Nchemba
 
Dkt. Nchemba amelipongeza Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania pamoja na madhehebu mengine ya dini kwa kushirikiana na Serikali kutoa huduma za kijamii kwa wananchi ikiwemo huduma za afya, elimu, maji na mambo mengine na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hizo za dini ili kuwahudumia wananchi.
 
Alisema kuwa KKKT inafanyakazi nzuri katika utoaji wa huduma kwa jamii upande wa elimu ambapo lina taasisi 120 za kielimu zikiwemo shule za Msingi 17-zinazotumia lugha ya Kiingereza kufundishia, Shule za sekondari 70, Vyuo vya Ufundi vya Kati 21 Vyuo Vikuu 6 na Shule Maalum 9 kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum maeneo mbalimbali nchini. kwa kukosa elimu.
 
“Ninatoa pongezi nyingi kwa KKKT kwa kuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma za afya, Nimeelezwa mnavyo vituo 172 vya kutolea huduma za afya ambapo mnazo hospitali 24, ikiwepo Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya kaskazini-KCMC, iliyopo Moshi Mkoani Kilimanjaro, pamoja na Vituo vya Afya/Zahanati 148, zilizopo katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Hongereni sana kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ‘’ aliongeza Dkt. NChemba
 
Kuhusu Demokrasia, Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kinara cha masuala ya demokrasia kwa vitendo.
 
Alieleza kuwa demokrasia imeimarika kwa kiwango kikubwa ambapo Serikali imeendelea kuwashirikisha wadau wote kujadili namna bora ya kuendesha shughuli za kisiasa hali iliyoleta muafaka na maelewano baina ya vyama vya siasa na wafuasi wa vyama hivyo.
 
Dkt. Nchemba alisema kuwa ni dhamira ya Serikali kuendelea kukuza na kuimarisha demokrasia ya vyama vya siasa, sambamba na kudumisha amani, utulivu na umoja wa kitaifa vilivyopo nchini. 
Alitoa wito kwa Viongozi wa madhehebu ya dini kuendelea kuhimiza na kuhubiri amani na utulivu nchini kwa faida ya vizazi vya sasa na kwa vizazi vijavyo na kuwahimiza waendelee kutoa mafundisho ya kiroho yenye msisitizo wa kuthamini amani ambayo nchi imepewa na Mwenyezi Mungu kwa kuwa pasipo amani hata ibada haziwezi kufanywa kwa utulivu
Akizungumza kwenye Ibada hiyo maalumu, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Askofu Dkt. Fredrick Shoo aliipongeza Serikali ya awamu ya Sita kwa jitihada kubwa za kuwaletea wananchi maendeleo na kwamba Kanisa linaunga mkono juhudi hizo.
 
Askofu Dkt. Shoo alisisitiza masuala kadhaa katika hotuba yake ikiwemo umuhimu wa wanasiasa na viongozi wa dini kuhimiza hifadhi ya mazingira kutokana na athari ambazo zimeanza kujitokeza na zitakazo endelea kujitokeza kutokana na uharibifu huo wa mazingira.
 
Pamoja na mambo mengine, alihimiza jitihada za kukabiliana na hali hiyo iwe kwa vitendo zaidi ili kulinusuru taifa kutokana na athari hizo za mabadiliko ya tabianchi na kushauri pia Serikali ibuni vyanzo mbadala vya nishati ikiwemo umeme jua na upepo.
 
Mwisho