Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

WAZIRI MKUU MAJALIWA AFANYA ZIARA OFISI YA SOKO LA HISA DAR ES SALAAM

26 Aug, 2025
WAZIRI MKUU MAJALIWA AFANYA ZIARA OFISI YA SOKO LA HISA DAR ES SALAAM

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, akigonga kengele kuashiria kuorodhoreshwa rasmi zaidi ya kampuni 28, katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), huku thamani ya soko (market capitalization) ikiwa imefikia zaidi ya TZS trilioni 22, na wawekezaji walioko kwenye akaunti zaidi ya 683,000, huku wengi wao wakiwa vijana na wanawake), hafla iliyofanyika katika Ofisi za DSE, jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya (wa tatu kulia), Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Bw. Peter Situmbeko, na wajumbe wa Bodi ya DSE.
 

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema kuwa Serikali imeweka Sera, Sheria na Taratibu zinazolenga kuchochea biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi nchini.

Hayo yamesemwa kwaniaba yake na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, akizungumza wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, katika Ofisi za Soko la Hisa la Dar es Salaam, Morocco, Jijini Dar es Salaam.

“Hatua hiyo ni alama ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, namna ilivyoweka mazingira wezeshi ya kisera, sheria na kiutendaji ikiwa ni msisitizo mkubwa katika kukuza uchumi shirikishi na jumuishi” Alisema Bw. Mwandumbya.

Aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha ilitunga Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21-2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji katika sekta ya umma na binafsi ambapo, Soko la Hisa la Dar es Salaam limeonesha ukomavu wa kuwa jukwaa la kisasa lenye uwazi  linalowaunganisha wawekezaji na kampuni zinazohitaji mitaji.

Alisema kuwa hivi sasa DSE imeorodhesha zaidi ya kampuni 28, thamani ya soko (market capitalization) ikiwa imefikia zaidi ya shilingi trilioni 22, na wawekezaji walioko kwenye akaunti wamefikia zaidi ya 683,000, wengi wao wakiwa vijana na wanawake.

 “Haya ni mafanikio makubwa yanayoonyesha ukuaji wa mwamko wa wananchi kushiriki katika uwekezaji na kuunganisha uchumi wa familia moja kwa moja na maendeleo ya Taifa” alisema Bw. Mwandumbya.

Aliongeza kusema kuwa katika kutengeneza mazingira bora ya kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 bado  Wizara ya Fedha na DSE wanayo nafasi kubwa ya kupanua wigo wa masoko ya mitaji na dhamana nchini na nje ya mipaka ya Tanzania kwa Kuhamasisha kampuni za bima, benki,  kampuni za mawasiliano, na sekta nyingine kuorodheshwa katika soko la hisa ili kukuza mitaji na kuchochea uchumi wa Tanzania.

“ Hatua hiyo pia itasaidia kuendeleza bidhaa mpya za kifedha kama  hati fungani za kijani (Green Bond)  Sukuk, na Mfuko wa uwekezaji wa mali isiyohamishika (Real Estate Investment Trusts-REITs), Kuimarisha mifumo ya kidigitali kama DSE Hisa Kiganjani, ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi ikiwemo diaspora na Kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa kikanda kuongeza ushiriki wa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi” Alisisitiza Bw. Mwandumbya.

Alisema kuwa moja ya maeneo muhimu ni kuimarisha sekta ya fedha na masoko ya mitaji, kwa kuwa ni injini ya kukusanya mitaji ya muda mrefu kwa ajili ya miradi ya maendeleo, kuthamini mchango wa masoko ya mitaji katika maendeleo na uchumi wa Taifa kwa ujumla

Akizungumza katika tukio hilo, pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, alitoa rai kwa watanzania kushiriki na kuwekeza katika Soko la Hisa kwa kuwa uwepo wa soko hilo nchini umekuwa chachu ya maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo kufungua fursa za uwekezaji wa moja kwa moja kwenye kampuni zenye tija na kuwezesha familia nyingi kupata mapato ya ziada.

Alisema kuwa Soko hilo Kwa wafanyabiashara, limekuwa chanzo cha upatikanaji wa mitaji ya haraka na ya gharama nafuu kwa ajili ya upanuzi wa shughuli za kibiashara na uboreshaji wa bidhaa na huduma.

“Soko la Hisa limechangia kukuza mapato ya kodi, limeongeza ushiriki wa wananchi katika uchumi, na limeimarisha uthabiti wa sekta ya fedha, zaidi ya hayo, soko limekuwa kichocheo cha kuhamasisha tabia ya uwekezaji na akiba kwa wananchi, jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya muda mrefu ya uchumi wetu” alisema Mhe. Majaliwa.

MWISHO