Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

WASTAAFU WANAOLIPWA NA HAZINA WAASWA KUEPUKA MATAPELI

04 Aug, 2025
WASTAAFU WANAOLIPWA NA HAZINA WAASWA KUEPUKA MATAPELI

Afisa Hesabu Mkuu, Kitengo cha Pensheni Wizara ya Fedha, Bi. Joyce Chacky, akifafanua kuhusu pensheni inayolipwa kwa was taafu wanaohudumiwa na Hazina kwa Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mara (WAMAKU LTD), Bw. Momangi Range (kulia) na Makamu Mwenyekiti Chama Kikuu cha Ushirika Mara Bw. Emanuel Ndege, walipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo na Uvuvi 2025. 

 

Wizara ya Fedha imeawaasa wastaafu wanaolipwa mafao na Hazina kujiepusha na jumbe kwa njia ya simu zinazotumwa na watu wasiojulikana zikiwaelekeza kutuma fedha ili kuhakikiwa kwani wanaweza kutapeliwa fedha zao na matapeli hao.

Akizungumza wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma, Afisa Hesabu Mkuu, Kitengo cha Pensheni Wizara ya Fedha Bi. Joyce Chacky, alisema kuwa hakuna zoezi la uhakiki wa wastaafu linalofanywa na Hazina pia hakuna zoezi la uboreshwaji wa pensheni kwa mstaafu mmoja mmoja.

‘‘Siku za karibuni Wizara imekuwa ikipokea malalamiko kadhaa kutoka kwa wastaafu kuombwa fedha kupitia mitandao ya simu ili wafanyiwe uhakiki na kurekebishiwa viwango vya pensheni, hizo taarifa sio sahihi hakuna gharama zozote anazotozwa mstaafu anayehudumiwa na Hazina,’’alisema Bi. Chacky.

Alifafanua kuwa Wizara ya Fedha inalipa mafao ya kustaafu na mirathi kwa watumishi waliostaafu wakiwa katika ajira yenye masharti ya kudumu na malipo ya uzeeni kwa waliokuwa hawachangii kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambao walistaafu kabla ya tarehe 30 Juni, 2004.

Bi. Chacky alisema, hakuna gharama zozote zinazohitajika Wizara ya Fedha kwa ajili ya kushughulikia mafao ya uzeeni na hivyo kusisitiza wasataafu kupuuza jumbe hizo kwa njia ya simu ya mkononi kwani watu hao ni matapeli.

‘‘Tunasisitiza kwa mstaafu anayepokea mafao kutoka kwetu kutoa taarifa kituo chochote cha polisi kilicho karibu naye pale anapoombwa fedha kwa ajili ya kupata huduma yoyote katika ofisi zetu,’’alisisitiza Bi. Chacky.

Alitoa rai kwa mteja yeyote mwenye maswali, maoni na madai kufika Ofisi ya Hazina Ndogo iliyopo Mkoani kwake na Wizara ya Fedha, Zanzibar au kupiga simu ya huduma kwa mteja namba 0262160000.

Wizara ya Fedha pamoja na Taasisi zilizo chini yake inashiriki katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo na Uvuvi 2025’’.

MWISHO.