Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

WANANCHI WAIPONGEZA SERIKALI KWA ELIMU YA FEDHA

24 Nov, 2022
WANANCHI WAIPONGEZA SERIKALI KWA ELIMU YA FEDHA

Wananchi wa Mkoa wa Mwanza wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuwapa elimu ya fedha ambayo itawawezesha kutumia huduma za fedha zilizo sahihi kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Wameeleza hayo jijini Mwanza baada ya kupata mafunzo mbalimbali yanayohusu masuala ya fedha walipotembelea maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayoendelea katika viwanja vya Rock City Mall jijini humo.

Wakielezea maadhimisho hayo walisema yamewapatia elimu muhimu pamoja na miongozo mbalimbali ambayo wataendelea kuitumia na kutoa elimu kwa watu wengine wakiwemo familia zao hususani katika kuandaa bajeti za familia pamoja na namna bora ya usimamizi wa mapato ya familia.  

Bw. Ayoub Naftari ni miongoni mwa wananchi waliopata mafunzo hayo ambaye alisema elimu waliyoipata itawezesha kuwa na nidhamu ya matumizi fedha ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima ili kufikia malengo waliyojiwekea.

“Elimu hii itatuwezesha kuanzisha miradi mbalimbali na kupata mikopo kwa ajili ya kukuza na kuendeleza miradi hiyo na kuchangia katika kupunguza umaskini na kukuza uchumi wa nchi kutokana na nidhamu ya matumizi ya fedha”, alisema Bw. Naftari.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi wengine wa mkoa huo na mikoa ya jirani kutembelea maadhimisho hayo yaliyoanza Novemba 21 na kuendelea hadi Novemba 26, 2022 ili waweze kunufaika na elimu pamoja na huduma zinazotolewa.

Naye Bi. Celestina Makala alisema maadhimisho hayo yamemuwezesha kupata huduma katika taasisi mbalimbali za fedha, Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS), wajasirimali mbalimbali pamoja na kufahamu fursa mbalimbali zinazotolewa na Sekta ya Fedha katika kukuza na kuimarisha biashara.

Alisema elimu waliyoipata katika maadhimisho hayo imewawezesha kuelewa haki na wajibu wao katika matumizi ya huduma za fedha pamoja na kupata uelewa wa namna ya kujiwekea akiba, kukopa, umuhimu wa bima, uwekezaji na namna bora ya kujiandaa kabla ya kustaafu.

“Tunaipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa Sekta ya Fedha nchini na nafurahi zaidi kuona vitabu ambayo vitasidia wananchi kupata elimu ya masuala ya fedha na kuwahamasisha kuweka akiba, hii itatujengea utamaduni mzuri ambao utasaidia kuwa na Taifa la watu wanaothamini fedha kwa maendeleo”, alibainisha.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema, aliwataka wananchi kuwa na matumizi sahihi ya fedha ikiwa ni pamoja na kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba na kutumia huduma rasmi za fedha ili kujikwamua kiuchumi.

Aliwahamasisha wananchi kuendela kutembelea maadhimisho hayo na kujipatia maarifa na miongozo mbalimbali ambayo inalenga kuongeza maarifa katika masuala ya fedha.

MWISHO.