Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

WANAFUNZI WA USAGARA WAPATIWA ELIMU YA FEDHA WIKI YA HUDUMA ZA FEDHA TANGA

23 Jan, 2026
WANAFUNZI WA USAGARA WAPATIWA ELIMU YA FEDHA WIKI YA HUDUMA ZA FEDHA TANGA

Kaimu Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Bi. Dionisia Mjema akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Usagara kuhusu elimu ya usimamizi wa fedha binafsi ikiwa ni maadhimisho ya tano, yenye kaulimbiu "Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi" yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, Jijini Tanga.

 

Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha imeendelea kutoa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali ya jamii mkoani Tanga, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, jijini Tanga, kwa lengo la kuwajengea wananchi uelewa wa masuala ya kifedha na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu katika darasa la Elimu ya Fedha, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Grace Muiyaza, alisema mafunzo hayo yanawalenga watumishi wa umma, wafanyabiashara wadogo, vikundi vya wajasiriamali, wananchi wa kawaida pamoja na wanafunzi kuanzia ngazi ya shule ya msingi, sekondari hadi vyuoni.

“Tuko hapa tunatoa mafunzo kwa makundi yote ya jamii ya Tanga. Lengo letu ni kuwajengea uelewa wa masuala ya kifedha na kuwawezesha kushiriki vizuri katika shughuli za kiuchumi,” alisema Bi. Muiyaza.

Alieleza kuwa katika darasa la siku hiyo, walikutana na wanafunzi wa Shule ya Msingi Usagara na kuwapatia elimu ya usimamizi wa fedha binafsi, akisisitiza kuwa elimu hiyo ni muhimu kwa watoto kwa kuwa nao hupata fedha kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo kwa wazazi wao.

“Watoto nao wanapata fedha kwa matumizi yao ya kila siku, hivyo ni muhimu wafundishwe mapema namna ya kusimamia fedha ili waweze kufikia malengo yao ya muda mfupi na mrefu,” aliongeza.

Bi. Muiyaza alisema darasa hilo lilikuwa shirikishi na wanafunzi walionesha uelewa mzuri kuhusu masuala ya msingi ya usimamizi wa fedha, hususan umuhimu wa kuweka akiba.

Alibainisha kuwa baadhi ya wanafunzi hupatiwa fedha nyingi zaidi ya mahitaji yao ya shule, hali inayowapa fursa ya kuanza utamaduni wa kujiwekea akiba mapema.

Katika hatua nyingine, alitoa wito kwa wazazi na walezi kuwalea watoto wao katika misingi sahihi ya kifedha, ikiwemo kutumia mifumo salama ya kutunza akiba badala ya njia zisizo salama kama vibubu au kuhifadhi fedha chini ya vitanda.

“Bado tunakutana na changamoto kubwa ya watu kuweka fedha kwenye sehemu zisizo salama na rasmi. Tunawahamasisha wazazi na jamii kwa ujumla kutumia benki, vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha, huduma za fedha kwa njia ya simu na kampuni za uwekezaji,” alisema.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Usagara, Salma Rajabu, alisema elimu aliyopata imemfungua macho kuhusu umuhimu wa kuweka akiba na kuhifadhi fedha sehemu salama.

“Hapo awali nilijua fedha zinawekwa kwenye kibubu au chini ya kitanda, lakini sasa nimejifunza kuwa ni salama zaidi kuweka benki au kwenye simu. Nitawaelimisha wazazi wangu na kuwaomba wanifungulie akaunti ya akiba,” alisema Salma.

Naye Hassan Mohamed, mwanafunzi wa darasa la sita katika shule hiyo, alisema somo hilo limemsaidia kuelewa umuhimu wa akiba kwa maisha ya baadaye na namna ya kuwashauri wazazi wao kutumia njia salama za kuhifadhi fedha.

Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanaendelea mkoani Tanga, yakilenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma za fedha na kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kwa makundi yote ya jamii.

Mwisho