Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

UMOJA WA ULAYA WAIPATIA TANZANIA MSAADA WA SHILINGI BILIONI 572

05 Jul, 2023
UMOJA WA ULAYA WAIPATIA TANZANIA MSAADA WA SHILINGI BILIONI 572

Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akishuhudia kusainiwa kwa mikataba mitatu yenye thamani ya shilingi bilioni 455.09 na msaada wa shilingi bilioni 117.04 kwa ajili ya utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023, katika Ukumbi wa Hazina (Treasury Square), jijini Dodoma. Kwa upande wa Serikali ulisainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (kulia) na Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Tanzania, Mhe. Manifredo Fanti. Anayeshuhudia upande wa kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb)

Na. Peter Haule, WFM, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameshuhudia Serikali yake ikisaini mikataba mitatu na Umoja wa Ulaya, nyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 455 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuendeleza sekta binafsi, na msaada wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha uliomalizika wa 2022/2023 wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 117.

Makubaliiano ya mikataba hiyo yamesainiwa jijini Dodoma kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Tanzania, Mhe. Manifredo Fanti, kwa niaba ya Umoja huo. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema kuwa Tanzania inatekeleza program ya kujenga kesho iliyobora kwa vijana na wanawake kwenye kilimo ambapo inatarajia kutumia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB), kufadhili vijana na wanawake watakaoshiriki katika mradi huo.

Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliuomba Umoja wa Ulaya kuangalia uwezekano wa kuziwezesha Benki mbili zinazomilikiwa na Serikali ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) kwa kuziwezesha kimtaji ili ziwezi kutoa mikopo kwa ajili ya kuendeleza kilimo na uwekezaji nchini, kama inavyofanyika kwa Benki nyingine za biashara.

Aidha, aliuomba Umoja wa Ulaya kutoa fedha kwa ajili ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza ili kuimarisha shughuli za usafirishaji kutokana na kukua kwa Jiji hilo na kuwa kitovu cha biashara.

Kwa Upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alisema mafanikio yaliyopatikana kutoka Umoja wa Ulaya yaliyotokana na kuimarika kwa ushirikiano ni pamoja na ufadhili wa dola za Marekani milioni 12 kati ya dola za Marekani milioni 67.87 zilizotengwa kwa ajili ya kuboresha viwanja vya ndege vya mikoa mitano ya Kigoma, Tabora, Bukoba, Sumbawanga, na Shinyanga.

Mafanikio mengine ni  upatikanaji wa Euro milioni 10 kwa ajili ya Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira wa Ziwa Victoria na kufanya jumla ya fedha zilizotolewa kwa mradi huo kufikia Euro milioni 45 ikiwa ni mkopo wa riba nafuu na kufunguliwa kwa fursa za usaidizi wa Umoja wa Ulaya kwa sekta binafsi ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na benki za biashara. 

Akizungumza awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya fedha na Mipango, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, alisema kuwa Programu zilizoibuliwa hadi sasa na ambazo zinatekelezwa kwa kipindi cha miaka minne ya awamu ya kwanza ni pamoja na  Mradi wa kuboresha masuala ya kijinsia na wanawake, wenye thamani ya Euro milioni 70 sawa na shilingi bilioni 177.25 unaotekelezwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. 

Vilevile mradi wa Uboreshaji wa sekta ya Tehama Serikalini wenye thamani ya Euro milioni 35 sawa na shilingi bilioni 88.62 unaotekelezwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Miradi mingine ni Uboreshaji Miji wenye thamani ya Euro milioni 75 sawa na shilingi bilioni 189.91 unaotekelezwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, uboreshaji wa utawala wa Fedha za Umma na sekta binafsi wenye thamani ya EURO milioni 63.35 sawa na shilingi bilioni 160.41 unaotekelezwa na Wizara ya Fedha na Mipango.

"Mradi mwingine ni ule wa Uchumi wa Buluu wenye thamani ya Euro milioni 110 sawa na shilingi billion 279.18 unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar na Mradi wa Kusaidia masuala ya ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya wenye thamani ya Euro milioni sita sawa na shilingi bilioni 15.19 unaotekelezwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya" Alisema Dkt. Mwamba

Kwa upande wa Zanzibar, chini ya programu ya kuboresha miji, itanufaika na ujenzi wa miundombinu ya kijamii katika Kisiwa cha Pemba ambapo Euro milioni 5 sawa na shilingi billioni 12.66 zimetengwa kwa ajili hiyo. 

Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Mhe. Manifredo Fanti, alisema kuwa kwa mwezi Juni na Julai Umoja huo utatoa shilingi biloni 140 kwa ajili ya kusaidia Bajeti, na pia wamesaini mikataba itakayonufaisha Uchumi wa buluu, kuwezesha sekta ya umma na binafsi na vifaa vya mafunzo ambayo kwa ujumla ina thamani ya Euro milioni 179.35 sawa na takribani shilingi bilioni 468 ambazo zitasaidia program hizo kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar kwa kipindi cha miaka minne.

Mhe. Balozi Fanti, amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kufanya mabadiliko ya kisera yanayolenga kuleta usawa wa kijinsia ambayo yanaungwa mkono na umoja huo.

Balozi huyo alitumia nafasi hiyo kuaga kwa kuwa anatarajia kuondoka Tanzania baada ya muda wake kumalizika na amesema kuwa Tanzania itafikia malengo yake ya maendeleo kutokana na jitihada zinazochukuliwa na alishukuru kwa ushirikiano mzuri alioupata Tanzania ambao umezaa matunda mazuri.

Mwisho.