Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

TANZANIA YAWASILISHA TAARIFA YA MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU (SDGS) UMOJA WA MATAIFA

19 Jul, 2023
TANZANIA YAWASILISHA TAARIFA YA MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU (SDGS) UMOJA WA MATAIFA

Tanzania imewasilisha Taarifa ya Pili ya Mapitio ya Hiari ya Nchi katika Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, katika Jukwaa la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa, ambapo taarifa hiyo imeonesha mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika utekelezaji wa Malengo hayo ikiwemo kuimarisha huduma za Jamii, miundombinu, mapambano dhidi ya umaskini na maradhi pamoja na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Taarifa hiyo imewasilishwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa niaba ya Serikali, katika Jukwaa hilo la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York nchini Marekani kwa njia ya video fupi na wasilisho hilo kusimamiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Taarifa hiyo ya Mapitio ya Hiari ya Nchi katika Utekelezaji wa malengo ya Maendeleo Endelevu  ilikuwa inawasilishwa kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 2019.

Alisema kuwa Serikali imeendelea kuweka programu na mipango mbalimbali ya kupiga vita umaskini, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, matumizi ya teknolojia, ujenzi wa miji salama, usawa wa kijinsia na mambo mengine kadha wa kadha, licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazohitaji kufanyiwa kazi kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa malengo hayo.

“Ripoti hii imeweka mikakati mbalimbali ya kufikia ajenda ya maendeleo ya 2030 kwa kuainisha masuala ya haki za binadamu, usawa wa kijinsia na namna ya kuwawezesha vijana kupitia mipango yetu ya maendeleo ya kitaifa” alisema Dkt. Nchemba

Alitaja baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa kuwa ni pamoja na ongezeko la upatikanaji wa maji safi na salama ambapo takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2021 wastani wa kiwango cha upatikanaji maji maeneo ya vijijini kilipanda hadi kufikia asilimia 74.3 ikilinganishwa  na mwaka 2019 kiwango hicho kuwa asilimia 70.1.

“Kuna ongezeko pia la upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme ambapo idadi ya watu wanaopata huduma hiyo imeongezeka kutoka asilimia 67.5 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 78.4 mwaka 2021.

Aidha, Dkt. Nchemba alieleza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji ambapo hivi sasa inatekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya umeme, viwanja vya ndege na barabara. Aidha, huduma za  afya, elimu na maji zimeendelea kuboreshwa, huku usalama wa chakula ukiendelea kuimarika pamoja na kuendelea na utekelezaji madhubuti programu mbalimbali za kupambana na umaskini.

Alisema kuwa Sekta ya utalii imeendelea kufanya vizuri licha ya changamoto za UVIKO -19 ambapo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alishiriki katika kutangaza utalii kupitia filamu  itwayo the Tanzania Royal Tour ambapo matokeo ya filamu hiyo yalipelekea idadi ya watalii kutoka nje ya nchi kuongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1,454,920 mwaka 2022, sawa ana ongezeko la asilimia 57.7

Dkt. Nchemba alisema kuwa tangu mwaka 2019 Serikali ilipowasilisha taarifa yake ya kwanza ya Mapitio ya Hiari ya Nchi katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu katika Jukwaa la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa. Nchi imepitia changamoto mbalimbali ikiwemo mlipuko wa UVIKO 19, vita vinavyoendelea baina ya Urusi na Ukraine, mabadiliko ya tabianchi pamoja na viwango vya juu vya riba vya mikopo ambapo vimeendelea kuonesha athari zake kwa Tanzania na nchi nyingine duniani. Aidha, Tanzania imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali katika  kukabiliana na hali hiyo.

Alitoa wito kwa Taasisi za fedha na Jumuiya ya kimataifa kuweka sera zitakazoongeza ufadhili, misaada na mikopo yenye masharti nafuu itakayosaidia nchi kupata fedha zitakazowezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikijumuisha miundombinu inayotegemea matumizi ya teknolojia, kuimarisha ubunifu, na kuongeza tija katika sekta ya kilimo ambayo ni tegemezi kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya vijana, na mwisho kuimarisha haki za wanawake na Watoto.

“Ninatoa wito kwa washirika wa ndani na jumuiya ya kimataifa kuiunga mkono Tanzania ili ifikie malengo yake kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu na ya muda mrefu, ili tuweze kutekeleza malengo ya SDGs, kukuza biashara kwa kuongeza mauzo nje ya nchi, kukaribisha wawekezaji, kuimarisha teknolojia na kubadilishana uzoefu” aliongeza Dkt. Nchemba

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba, alisema kuwa Tanzania itaendelea kuongeza bajeti yake katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu 2030 ambapo lengi kuu ni kuhakikisha watu wanapata maendeleo na nchi inakua kiuchumi kwa ajili ya manufaa ya wananchi wote hususan vijana na kwamba Mkutano huo wa Jukwaa la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa umeiwezesha Tanzania kupata uzoefu wa namna nchi nyingine zilivyoweza kukabiliana na changamoto hiyo ya kusukuma maendeleo yao licha ya vikwazo mbalimbali vinavyoikabili dunia hivi sasa.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 39 kati ya 193 ya wanachama wa Umoja wa Mataifa zilizopata fursa ya kuwasilisha taarifa  hiyo. Aidha, Ujumbe wa kutoka Tanzania umetumia nafasi hiyo katika kushiriki mikutano ya pemebezoni ya Mkutano huo katika  kubadilishana uzoefu na nchi nyingine zilizoshiriki mkutano huo muhimu.