Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

TANZANIA YASAINI MKATABA WA BILIONI 988 KUENDELEZA MIUNDOMBINU JIJINI DAR ES SALAAM

21 Feb, 2024
TANZANIA YASAINI MKATABA WA BILIONI 988 KUENDELEZA MIUNDOMBINU JIJINI DAR ES SALAAM
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (kulia), na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Bw. Nathan Belete, wakionesha hati ya mkataba  wenye thamani ya Euro milioni 361.1 (sawa na takribani shilingi bilioni 988.093) kwa ajili ya kutekeleza Awamu ya Pili ya Mradi wa Kuendeleza Miundombinu Dar es Salaam (Dar Es Salaam Metropolitan Development Project Phase II (DMDP II). Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Hazina Ndogo, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb), Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Khamis Hamza Khamis, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mwenyekiti wao Dkt. Faustine Ndugulile, Viongozi waandamizi wa Serikali pamoja na Viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
 
 
Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia zimesaini mkataba wenye thamani ya Euro milioni 361.1 (sawa na takribani shilingi bilioni 988.093) kwa ajili ya kutekeleza Awamu ya Pili ya Mradi wa Kuendeleza Miundombinu Dar es Salaam {Dar Es Salaam Metropolitan Development Project Phase II (DMDP II)}.
 
Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika jijini Dar es Salam kati ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete.
 
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema DMDP II itaendelea kuboresha miundombinu muhimu ya umma katika Wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni zilizokuwepo kwenye Awamu ya I ya mradi huo, sambamba na kupanua wigo wa uboreshaji miundombinu katika Wilaya zinazoingia katika mradi kwa mara ya kwanza za Ubungo na Kigamboni.
 
Alisema lengo la mradi huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2020 -2025 na ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayolenga kutanua na kuboresha miundombinu na huduma katika Jiji la Dar-es-Salaam.
 
“Hii ikijumuisha ujenzi na uboreshaji wa mtandao wa barabara katika kupunguza msongamano na kuimarisha mawasiliano, mitaro ya maji katika kupunguza athari za mafuriko pamoja na miundombinu ya masoko katika kutoa fursa za biashara na shughuli za kiuchumi ili kuboresha maisha ya wakazi wa Dar es Salaam”, alibainisha Dkt. Nchemba.
 
Aidha, Mhe.Dkt. Nchemba alisema Awamu ya Pili ya Mradi huo imezingatia ustahimilivu wa athari za mabadiliko ya tabianchi katika ujenzi wa miundombinu, miradi rafiki kwa mazingira na yenye lengo la kusaidia na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete alisema Benki hiyo inajivunia kuwa sehemu ya ukuaji wa Dar es Salaam ambapo katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, benki hiyo imetenga dola bilioni 1.5 kwa ajili ya ufadhili maendeleo ya jiji hilo.
 
Alisema mfano mzuri wa matokeo ya ushiriki wao katika maendeleo ya Dar es Salam unaonekana katika matokeo ya Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Kuendeleza Miundombinu Dar es Salaam wa dola milioni 300 uliokamilika mwaka jana.
 
“Mradi huu ulijenga kilomita 207 za barabara na vituo vinne vya mabasi ambavyo vimeboresha usafiri kwa zaidi ya watu milioni 3.5 na kujenga kilomita 75 za mfumo wa maji na mabwawa matatu ya kuzuia mafuriko, kupunguza mafuriko kwa watu wanaoishi katika eneo la hekta 400 lenye hatari ya mafuriko”, alisema Bw. Belete.
 
Aliongeza kuwa mradi huo pia ulijenga masoko 10 na maeneo 6 ya wazi ya wananchi kupumzika, kutoa fursa za kiuchumi na upatikanaji wa bidhaa na kufanya jiji kuwa mahali pazuri zaidi pa kuishi.
 
Bw. Belete alibainisha kuwa mradi huo pia ulianzisha mifumo ya kuongeza uwezo wa Serikali za Mitaa kuboresha ukusanyaji wa mapato, kutekeleza udhibiti wa maendeleo pamoja na kupanga na kudumisha miundombinu.
 
Naye Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa, alisema Wizara hiyo itasimamia kikamilifu mradi huo na kuhakikisha unatekelezwa kwa wakati.
 
Alisema mradi huo unalenga kujenga kimlomita 250 za Barabara, kutokomeza changamoto ya taka ngumu, kujenga masoko ya kisasa 18, vituo vya mabasi tisa pamoja na mifereji mikubwa ya maji ya mvua ili kupunguza adha ya mafuriko jijini Dar es Salaam.
 
Akizungumza kwa niaba ya Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Wabunge wa mkoa huo na Mbunge wa Kigamboni, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile, aliishukuru Serikali na Benki ya Dunia kwa kuwasikiliza na kutimiza ahadi yao ya hakikisha fedha hizo zinapatikana.
 
Mhe. Ndugulile alisema Awamu ya Pili ya Mradi wa Kuendeleza Miundombinu Dar es Salaam ni muhimu kwa maendeleo ya nchi kwa kuwa asilimia 70 ya mapato ya Serikali yanatoka  jiji hilo.
 
Aliiomba mamlaka husika kuhakikisha mradi huo unaanza kwa haraka na kuahidi  kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati na unaendana na fedha zilizotolewa.
 
Mwisho.