Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

TANZANIA YAMALIZA MUDA WAKE WA KUONGOZA VIKAO VYA IMF KWA MAFANIKIO MAKUBWA

17 Oct, 2022
TANZANIA YAMALIZA MUDA WAKE WA KUONGOZA VIKAO VYA IMF KWA MAFANIKIO MAKUBWA

TANZANIA imemaliza muda wake wa miaka miwili wa kuwa Mwenyekiti wa Kundi la Kwanza la Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency) katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), linalojumuisha Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi 23 za Afrika, ambapo katika muhula wake, mafanikio makubwa yamepatikana, licha ya kukabiliwa na changamoto za UVIKO-19 na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine.

 

Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema hayo Jijini Washington D.C, nchini Marekani, baada ya kuongoza mkutano wake wa mwisho Mawaziri  na Mgavana wa Kundi hilo na kukabidhi rasmi uongozi wa miaka mingine miwili kwa Namibia kama Mwenyekiti na nchi ya Botswana kama Makamu Mwenyekiti.

 

Katika kipindi cha uongozi wa Tanzania, Kundi hilo limenufaika kwa ongezeko la upatikanaji wa rasilimali fedha kwa nchi wanachama wake na kuwa na sauti zaidi katika shughuli za uendeshaji za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).  

 

Nafasi ya Tanzania katika kundi hilo iliwezesha kuimarisha mashirikiano kati yake na IMF ambapo imeshudiwa Shirika hilo likiongeza uwekezaji wake nchini kwa takriban shilingi trilioni 1.3. zilizotolewa kama mkopo usio na riba kwa ajili ya kukabiliana na athari za UVIKO-19 katika sekta za elimu, afya, maji na utalii hivi karibuni.

 

Aidha, katika kipindi hicho, IMF iliidhinishia Tanzania mkopo nafuu wenye thamani ya jumla ya shilingi trilioni 2.7 za kukabiliana na athari za UVIKO-19 na vita ya Ukraine ambapo tayari kiasi cha shilingi bilioni 347 zimeshatolewa ili kuleta ahueni kwa wanachi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini. 

 

Alisema kuwa ajenda kubwa ya mkutano huo ambao aliuongoza kwa mara ya mwisho, ilijikita katika kutafuta namna IMF inavyoweza kuzisaidia nchi wanachama kukabiliana na uhaba wa chakula  na mfumuko wa bei uliosababishwa na athari za UVIKO-19, vita vya Urusi na Ukraine na mabadiliko ya tabia nchi.

 

Dkt. Nchemba alilita Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuendelea kushirikiana na uongozi mpya wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka Kundi la Kwanza la nchi za Afrka, kwa kutoa mikopo na misaada itakayosaidia kufufua uchumi na kukabiliana na uhaba wa chakula katika nchi hizo.

 

Aidha, Dkt. Nchemba, alitoa wito kwa nchi wanachama wa Kundi hilo kuwa na sauti moja ya kupigania maslahi ya nchi zao katika Shirika hilo kubwa la Fedha la Kimataifa na kuhakikisha wanatunga sera rafiki zitakazoimarisha sekta za uzalishaji, hususan kwenye kilimo. 

 

Mwisho