Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

TAFITI ZENYE TIJA ZITATATUA CHANGAMOTO ZA KIUCHUMI

28 Oct, 2025
TAFITI ZENYE TIJA ZITATATUA CHANGAMOTO ZA KIUCHUMI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo (Katikati), akikata utepe kuzindua Mwongozo wa Tafiti na Ubunifu wa Wizara ya Fedha, wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Kamati za Utafiti na Ubunifu, Kamati Elekezi, na Kamati ya Kiufundi, iliofanyika katika Ukumbi wa Kambarage,Treasury Square, jijini Dodoma. Wengine katika picha ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mipango Wizara ya Fedha, Bw. Alex Mwakisu (kushoto) na Kaimu Kamishna Msaidizi wa Sera sehemu ya Utafiti na Modeli za Kifedha, Dkt. Iddy Zuberi Kayumba (kulia).

 

Wajumbe wa Kamati za Utafiti na Ubunifu, Kamati Elekezi, na Kamati ya Kiufundi wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwazi na ubunifu ili kuhakikisha kuwa tafiti zinazofanyika zinatoa mapendekezo yanayotekelezeka.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, wakati akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, katika uzinduzi rasmi wa Kamati za Utafiti na Ubunifu, Kamati Elekezi, na Kamati ya Kiufundi uliofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.

Bi. Omolo alieleza kuwa Wizara ya Fedha inatambua kuwa utafiti na ubunifu ni injini ya maendeleo endelevu na msingi wa mageuzi ya kisera, kiuchumi na kiutendaji.

Alifafanua kuwa kuanzishwa kwa Kamati Elekezi na Kamati ya Kiufundi ni sehemu ya utekelezaji wa Mwongozo wa Utafiti na Ubunifu wa Wizara ya Fedha (2025), ambao umeweka mfumo rasmi wa kuratibu shughuli hizo ndani ya Wizara.

“Kupitia utafiti na ubunifu, Wizara inaweza kubaini changamoto, kuibua fursa mpya na kubuni suluhisho endelevu katika maeneo ya sera, bajeti, ukusanyaji mapato, matumizi ya fedha za umma na usimamizi wa uchumi kwa ujumla,” alisema Bi. Omolo.

Akielezea majukumu ya kamati hizo, Bi. Omolo alisema kuwa Kamati Elekezi itakuwa na jukumu la kuchambua mawazo ya utafiti na ubunifu, kupitia taarifa za tafiti, kupendekeza motisha kwa wabunifu, na kusimamia ubora wa utekelezaji wa tafiti hizo.

“Uteuzi wenu umezingatia uzoefu, weledi na uwezo wenu kiutendaji katika taasisi/idara mnazozitumikia.” aliongeza Bi. Jenifa

Kwa upande mwingine, Kamati ya Kiufundi itakuwa na jukumu la kuchambua mawazo ya tafiti na bunifu, kuhakikisha ubora na uzingatiaji wa maadili ya utafiti, pamoja na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa Kamati Elekezi kwa ajili ya hatua zaidi.

Kwa niaba ya wajumbe wa kamati hizo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mipango katika Wizara ya Fedha, Bw. Alex Mwakisu, aliahidi kuwa watafanya kazi kwa ushirikiano na kwa wakati ili kuhakikisha kuwa tafiti na bunifu zinazofanyika zinakuwa na mchango chanya kwa Serikali na Taifa kwa ujumla.

Kamati ya Kiufundi ya Utafiti na Ubunifu inaundwa na wajumbe ambao ni Dkt. Remidius D. Ruhinduka, Bw. Ernest K. Laiton, Dkt. Iddy Zuberi Kayumba, Bw. Innocent Anthony, Dkt. Lusekelo Mwandondwa, Bi. Catherine Karumuna, Bi. Nacky Sinda, Dkt. Lusajo Mwankemwa, na Deogratius Protas Massawe.

Kamati Elekezi ya Utafiti na Ubunifu inaundwa na Bw. Moses W. Dulle, Dkt. Remidius D. Ruhinduka, Bw. William M. Mhoja, Bi. Veronica M. Kishala, Bw. Fundi M. Makama, Bw. Kishiwa Y. Masabo, Bw. Ernest K. Laiton, Bi. Emma Komba, Bi. Dionisia P. Mjema, Bw. Massaga J. Fimbo, Dkt. Deogratius P. Macha, na Bw. Seif Kuchengo

MWISHO.