Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

SERIKALI YATOA BILIONI 50 KWA HALMASHAURI 55 KUPANGA NA KUMILIKISHA ARDHI

12 Nov, 2021
SERIKALI YATOA BILIONI 50 KWA HALMASHAURI 55 KUPANGA NA KUMILIKISHA ARDHI

Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imeipatia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi shilingi bilioni 50 kwa ajili ya kuzikopesha Halmashauri 55 kutekeleza Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi nchini.

Hafla ya utiaji Saini wa hati ya makubaliano ya fedha hizo imefanyika Jijini Dodoma kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi (Mb) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Ummy Mwalimu (Mb).

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alisema utekelezaji wa programu hiyo ni muhimu kwa Serikali hususani Wizara ya Fedha kwa kuwa utatengeneza chanzo kipya cha kodi kwa miaka inayokuja.

“Mpango huu utatupeleka katika hatua kubwa zaidi, tutaimarisha shughuli za uzalishaji kwa kutumia ardhi pamoja na kutatua migogoro ya ardhi ambayo imekuwa kero kwa muda mrefu”, alifafanua Dkt. Nchemba.

Aidha aliziagiza Halmashauri zote zilizopata mkopo huo kuzitumia fedha hizo kwa kufuata miongozo, sheria na maelekezo yaliyowekwa ili kufanikisha malengo yaliyo kusudiwa na kuwa mfano bora kwa wengine wanaohitaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) aliipongeza Serikali kwa kutoa fedha hizo ambazo zitawezesha utekelezaji wa kipaumbele cha wizara hiyo cha kuendeleza miji na vijiji.

Aliahidi kuzisimamia fedha hizo kikamilifu kwa kuhakikisha zinatumika kwa malengo kusudiwa na kubainisha kuwa programu hiyo italeta matokeo chanya kwa kupunguza uendelezaji na ukuaji holela wa miji, kupendezesha mitaa na kuwa safi na salama pamoja na kuongeza maeneo ya ardhi kwa ajili ya miundombinu ya kijamii na kiuchumi.

Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi (Mb) alisema fedha hizo zikitumika vizuri zitalipwa kwa wakati kwa kuwa zitaziwezesha Halmashauri kiuchumi na kupata faida ya takribani shilingi bilioni 41 ndani ya miezi sita.

alisema pamoja na kuziwezesha halmashauri, fedha hizo pia zitatumika kutatua kero na dhuluma kwa wananchi na kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwa wamiliki wa maeneo yaliyopimwa na kupangwa ni rahisi kukopesha kuliko wanaomiliki maeneo yasiyo rasmi.

Aliwaagiza Wakurugenzi wote wanaopata fedha hizo kutatua changamoto mbalimbali za fidia kwa wananchi wanaochukuliwa ardhi na kuwataka kuhakikisha wanatumia fedha hizo kuwalipa wananchi fidia kabla ya kuchukua maeneo yao.

Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanueli Tutuba alisema utoaji wa fedha hizo ni utekelezaji wa majukumu ya wizara na kubainisha kuwa miongoni mwa majukumu ya msingi ya Wizara ya Fedha na Mipango ni kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza mipango ya Serikali inayowezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, kuimarisha shughuli za uchumi na ustawi wa jamii, pamoja na kusimamia matumizi bora ya fedha za umma.

Fedha hizo zimetolewa kwa Halmashauri 55 zilizokidhi vigezo kati ya 78 zilipeleka mapendekezo, zilizopata fedha hizo ni pamoja na Dodoma Jiji shilingi bilioni tatu, Ilemela shilingi bilioni 3.5, Chalinze shilingi bilioni mbili na Meru shilingi bilioni 6.5.