Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

RASILIMALI WATU NA FEDHA VYAPEWA KIPAUMBELE SADC

14 Aug, 2023
RASILIMALI WATU NA FEDHA VYAPEWA KIPAUMBELE SADC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) (kulia) akifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Luanda, Angola, ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliopangwa kufanyika Agosti 17, 2023. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban.

 

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imejipanga kuwekeza katika rasilimali watu na fedha ili kuchochea maendeleo ya sekta ya viwanda ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Tamko la Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu uwekezaji huo lililotolewa jijini Dar Es Salaam mwezi Julai 2023.

Hayo yamebainishwa jijini Luanda, Angola na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) kwenye Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC ulioshirikisha nchi 16 wanachama wa jumuiya hiyo.

Dkt. Tax alisema kuwa tamko la Dar Es Salaam limeainisha masuala mbalimbali ya utekelezaji kwa ajili ya kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu ambayo yameendelea kujadiliwa katika Mkutano wa 43 wa SADC ili kuhakikisha kuwa, katika kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu ambayo inahusu umuhimu wa rasilimali watu na fedha katika maendeleo endelevu ya viwanda, tamko la Dar Es Salaam linakuwa sehemu ya utekelezaji wa kaulimbiu hiyo.

“Suala la uwekezaji katika rasilimali watu, suala la uendelezaji wa rasilimali watu katika kuendeleza uchumi, ni vitu ambavyo tunaendelea kuvisukuma kama ilivyokuwa kwenye mkutano jijini Dar es Salaam ambapo Rais wetu alikuwa Mwenyekiti wa mkutano ulioangazia masuala ya rasilimali watu uliofanyika Tanzania”, alieleza Dkt. Tax.

Awali wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC, Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Bw. Elias Magosi alisisitiza umuhimu wa nchi za SADC kuondoa vikwazo vinavyorejesha nyuma kasi ya muingiliano, uendelezaji wa viwanda na upatikanaji wa masoko lakini pia nje ya nchi hizo.

Alisema kuwa uondoaji wa vikwazo hivyo, utaifanya kanda ya SADC kuwa katika nafasi nzuri ya kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Mpango Elekezi wa Maendeleo ya Kikanda wa 2020-2030 na dira ya kanda hiyo ya 2050.

Alisema kuwa, licha ya changamoto zinazoikabili dunia, kama mabadiliko ya tabianchi na mgogoro wa Urusi na Ukraine ambazo zimesababisha athari nyingi kwenye Kanda ya SADC, Jumuiya hiyo imefanikiwa kuziwezesha nchi wanachama kupata masoko ya kikanda na kimataifa ambapo nchi zilizonufaika na masoko hayo ni pamoja na Tanzania ambayo ilipata soko la parachichi katika nchi za China, India na Afrika Kusini. 

Bw. Magosi aliendelea kueleza kuwa, kwa uratibu wa Sekretarieti ya SADC, nchi wanachama zimefanikiwa kupunguza msongamano wa magari, muda na gharama za usafirishaji katika baadhi ya mipaka, hususan yenye vituo vya pamoja vya mipakani (one stop border post-OSBP) kama Nakonde/Tunduma kwenye mpaka wa Tanzania na Zambia.

Kwa upande mwingine, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekabidhi uenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa Angola.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri ulitanguliwa na vikao vya wataalam ambapo kwa Tanzania viliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban. Aidha mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliopangwa kufanyika Agosti 17, 2023.

 

Mwisho.