Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

NCHI ZA AFRIKA ZAKUBALIANA KUTUMIA TEKNOLOJIA KUONGEZA MAPATO

06 Mar, 2024
NCHI ZA AFRIKA ZAKUBALIANA KUTUMIA TEKNOLOJIA KUONGEZA MAPATO

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, akiagana na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. Simon Sirro (kushoto), baada ya kumalizika kwa mkutano wa 56 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi Afrika, unaoratibiwa na Kamisheni ya Uchumi wa Afrika chini ya Umoja wa Mataifa (UNECA), uliofanyika Victoria Falls, Zimbabwe.

 

Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi wa nchi za Afrika wamekubaliana kuhakikisha wanakusanya na kutumia rasilimali zilizopo vizuri pamoja na kuboresha matumizi ya teknolojia ili kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Hayo yamesemwa Mjini Victoria Falls, Zimbabwe na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 56 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi kutoka Afrika unaoratibiwa na Kamisheni ya Uchumi wa Afrika chini ya Umoja wa Mataifa (UNECA)

Bw. Mwandumbya alisema kuwa kupatikana kwa rasilimali za kutosha kutawezesha Serikali kuhudumia miradi, kutimiza malengo ya kibajeti pamoja na kulipa madeni ya Serikali.

“Tumekuwa na sauti ya pamoja ya kuhakikisha tunaboresha Sheria, kanuni na usimamizi wa taasisi zetu za kukusanya mapato ili kuhakikisha tunaongeza mapato zaidi kutoka kwenye vyanzo vyetu, kwa kuwa upatikanaji wa rasilimali kutoka nje kwa njia ya mikopo na misaada imekuwa na changamoto kubwa,”alisema Mwandumbya

Bw. Mwandumbya alifafanua kuwa katika mkutano huo imewekwa mikakati mbalimbali itakayosaidia kujenga uwezo kwenye taasisi zilizopo ndani ya nchi za Afrika ili kuwa na uwezo thabiti wa kufanikisha malengo ya nchi husika.

“Tanzania tunaichukua hii kama ni sehemu ya kuboresha ubunifu wetu katika kazi zetu za kila siku, kuweza kuhakikisha mikakati ambayo imewekwa na uzoefu tulioupata kutoka kwa wenzetu, tunaenda kuutumia kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi katika maeneo ya kazi na kuweza kushauri Serikali namna ya kuenenda ili kuongeza zaidi ukusanyaji wa mapato ya Serikali”, alisema Mwandumbya.

Mkutano huo wa 56 uliojumuisha Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi chini ya uratibu wa Umoja wa Mataifa (UNECA) umehitimishwa kwa kukubaliana kutekeleza yote yaliyoafikiwa kwa pamoja ili kuwa na Uchumi imara na kuweza kupata rasilimali za kulipa madeni.

Mwisho