Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

MWANDUMBYA: TUTAENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA NCHINI

24 Nov, 2025
MWANDUMBYA: TUTAENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA NCHINI

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, akimkabidhi Zawadi ya cheti mmoja wa wahitimu wa Chuo Cha Kodi (ITA), waliofanya vizuri zaidi katika masomo mbalimbali, Adili Juma Salum, katika Mahafali ya 18 ya Chuo cha Kodi yaliyofanyika katika Ukumbi wa Multipurpose, jiji Dar es salaam.

 

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini na uwekezaji na kuitaka iendelee kutekeleza wajibu huo wenye tija.

Ameyasema hayo kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati wa Mahafali ya 18 ya Chuo cha Kodi cha TRA yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam jana.

Katika Mahafali hayo Mwandumbya, alisema kuwa TRA imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kukusanya mapato yatokanayo na kodi yanayosaidia kwa kiasi kikubwa kuendesha nchi kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii huku Chuo Cha Kodi kikitumika kuwapika watumishi wa Mamlaka hiyo na kuwafanya wawe bora zaidi.

Alisema TRA imechangia kwa kiasi kikubwa utulivu wa biashara uliopo nchini ambao pia unaletwa na amani na utulivu na kuongeza kuwa suala la amani siyo la kisiasa ni suala la uchumi na lina uhusiano wa moja kwa moja na maisha ya wananchi.

Aidha, aliunga mkono kauli iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Bw.  Yusuph Juma Mwenda, kuhusu kuongeza mapato yatokanayo na kodi kwa kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi na kuongeza wigo wa kodi huku walipakodi wazuri wakiwekewa mazingira rafiki.

Katika hotuba yake Kamishna Mkuu Mwenda, alirejea hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akilizindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa anataka Tanzania ijitegemee kiuchumi kwa kiasi kikubwa na kwamba kujitegemea hakuhusiani na kuongeza viwango vya kodi bali kuziba mianya ya ukwepaji kodi ili kuongeza mapato kwa maendeleo ya Taifa.

"Ieleweke kwamba nchi kujitegemea kwa kiasi kikubwa kiuchumi hakuhusiani na ongezeko la viwango vya kodi, tunachokifanya ni kuongeza juhudi katika kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kuongeza wigo wa kodi kwa kusajili walipakodi wapya" alisema Kamishna Mwenda.

Alisema kuwa anaamini wahitimu hao wa Chuo Cha Kodi watakuwa mabalozi wa kuongeza ulipaji kodi wa hiari ili kuleta ustawi wa biashara nchini ambao unategemea kwa kiasi kikubwa amani na utulivu.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, Bw. Uledi Mussa Abbas aliwataka wahitimu hao kuhamasisha jamii kuendelea kulipa kodi kwa hiari kwani ulipaji wa kodi ni Uzalendo.

Alisema kuwa anatamani Chuo Cha Kodi kiwe kitovu cha umahiri cha masuala ya Kodi na Forodha Barani Afrika kutokana na ubora wa hali ya juu wa mafunzo yanayotolewa na Chuo hicho.

Katika mahafali hayo yaliyohusisha wahitimu 561 baadhi ya wahitimu waliofanya vizuri wametunukiwa vyeti na kupatiwa zawadi mbalimbali huku wahadhiri waliofanya tafiti mbalimbali nao wakitunukiwa vyeti na zawadi.

Mwisho