Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

MAONI YA MABORESHO SERA YA KODI KURAHISISHA ULIPAJI KODI

27 Nov, 2023
MAONI YA MABORESHO SERA YA KODI KURAHISISHA ULIPAJI KODI

Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja, akieleza kuhusu umuhimu na mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wakati wa Kongamano la Jukwaa la Wafanyabiashara Mkoa wa Shinyanga ambapo Wizara ya Fedha ilitumia fursa hiyo kukusanya maoni ili kuweza kuboreshaji utozaji Kodi kwa mwaka 2024/25.

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amewataka wafanyabiashara kutoa maoni ya uboreshaji wa Sera za Kodi kupitia Timu ya wataalamu wa Uchambuzi wa Sera za Kodi kutoka Wizara ya Fedha ili waweze kulipa kodi kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Rai hiyo imetolewa Mkoani Shinyanga wakati wa Kongamano la Jukwaa la Wafanyabiashara lililoandaliwa na Mkoa huo ambalo lilitumika kukusanya maoni ya Uboreshaji wa Sera ya Kodi kwa mwaka wa Fedha 2024/25

Dkt. Abdallah, alisema kuwa eneo muhimu katika ufanyaji biashara ni Kodi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anawataka watu walipe kodi lakini Mamlaka za kukusanya kodi zikusanye kodi kwa weledi bila kuleta mgongano.

“Kodi haikusanywi kwa mtutu wa bunduki kwa kuwa anaekwenda kukusanya kodi haendi kukamata mhalifu na anaelipa kodi anapaswa kujua analipa kwa mujibu wa sheria na analipa kodi kwa sababu kodi ndio maendeleo ya nchi”, alisema Dkt. Abdallah.

Alisema kuwa Wizara ya Fedha iendelee kutoa elimu kwa walipa kodi ili wajue wanapaswa kulipa kodi namna gani ili kutengeneza mahusiano ya wafanyabiashara na Serikali.

Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja, alisema kuwa kwa pamoja kunatakiwa kuwekwa mikakati ya kuendelea kurasimisha biashara, kuhamasisha kutumia mashine za kielektroniki katika utoaji wa risiti na kuibua vyanzo vipya vya mapato ili kupunguza utegemezi wa mikopo kutoka nje ya nchi.

Aidha, alisema kuwa zipo kodi ambazo zililalamikiwa na wananchi hususani kodi ya miamala, Serikali ilisikia na kuondoa kodi hiyo unapotuma pesa, jambo linalodhihirisha kuwa Serikali ni sikivu hasa inapopata maoni ya walipakodi kuhusu utozaji kodi

Bw. Mhoja vilevilea alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hssan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatambua mchango wa Sekta Binafsi katika uwekezaji hivyo imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ili iweze kukuza uchumi wa nchi.

Alisema kuwa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu wezeshi ya usafirishaji na Nishati, kuhakikisha uhimilivu wa viashiria vya uchumi jumla na kuwa na sera za kodi zinazotabirika na kuwianisha tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Wizara na Mamlaka za Udhibiti.

Naye Meneja wa Usajili wa Malalamiko ya Kodi wa Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), Bi. Naomi Mwaipola, aliwataka wafanyabiashara na wadau waitumie taasisi hiyo ambayo inajitegemea kwa kuleta malalamiko ya kikodi ili kuweka mazingira ya haki na usawa.

“Unapoona hujatendewa haki unatakiwa kufika kwenye taasisi yetu bila kutozwa gharama tofauti tofauti na unapotumia Mahakama, lengo ni kumfanya mlipa kodi asiwe na manung’uniko yoyote” alisema Bi. Mwaipola.

Naye Mwenyekiti Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Shinyanga, Bw. Jonathan Manyama, ameiomba Serikali kuwa na uwazi katika utozaji kodi ili wafanyabiashara wajue kama kodi hizo zinafika eneo lilokusudiwa.

Amesema Wafanyabiashara wataendelea kulipa kodi kwa kuwa wanatambua kuwa ndio chanzo cha uboreshaji wa sekta mbalimbali zikiwemo za afya, miundombinu ya barabara, elimu na nishati.

Timu ya Wataalam wa Uchambuzi wa Sera za Kodi kutoka Wizara ya Fedha imeendelea na ukusanyaji wa maoni kwa wananchi Kikanda ili kuboresha Sera ya utozaji kodi kwa mwaka wa Fedha 2024/25, ambapo mikoa wa Arusha, Mwanza na Shinyaka imefikiwa.

 Mwisho.