Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

MAAFISA MASUULI WATAKIWA KUONDOSHA MALI CHAKAVU KUFIKIA SEPTEMBA 2025.

18 Jul, 2025
MAAFISA MASUULI WATAKIWA KUONDOSHA MALI CHAKAVU KUFIKIA SEPTEMBA 2025.

Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Serikali, Wizara ya Fedha Bw. Chotto Sendo (katikati) Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Bw. Edward Mwakipesile, (wa pili kulia) na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali Wizara ya Fedha Bw. Ismael Ogaga (wa pili kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa Masuuli baada ya kuhitimishwa kwa Mafunzo ya Usimamizi wa Mali za Umma kwa Maafisa Masuuli, yaliyoandaliwa na Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, mkoani Njombe. Mafunzo hayo yalihusisha Maafisa Masuuli kutoka katika mikoa mitano (5) ya Iringa, Songwe, Mbeya, Njombe, Ruvuma, yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkoa wa Njombe. Kulia ni Msimamizi wa Mali mkoa wa Njombe Bw. Maximilian Manamba na kushoto ni Kaimu Mkuu wa Hazina Ndogo mkoa wa Njombe Bw. Fortunatus Kanoni.

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, ameagiza Maafisa Masuuli nchini kuhakikisha kuwa mali zote za umma ambazo ni chakavu, sinzia na ziada na zilizokwisha matumizi zinaondoshwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo kufikia tarehe 30 Septemba, 2025.

Maagizo hayo yametolewa kwa niaba yake mkoani Njombe, na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Chotto Sendo, wakati akifungua Mafunzo ya Usimamizi wa Mali za Umma kwa Maafisa Masuuli. 

Bw. Sendo alisema kuwa kuelekea kuanza rasmi mwezi wa kwanza wa mwaka wa fedha 2025/2026, Maafisa Masuuli kwa kushirikiana na Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali ni vema kuzingatia kuwa mali zilizokwisha matumizi zinaondolewa kwa wakati.

‘‘Kumekuwa na changamoto ya uwepo na mlundikano wa mali chakavu, sinzia, ziada na zilizokwisha muda wa matumizi ikiwemo kemikali na dawa zilizoharibika na kuisha muda wa matumizi, utunzaji usioridhisha wa mali, hivyo mali hizo zifanyiwe utaratibu wa kuondoshwa kwa kufuata Kanuni, Sheria na Taratibu‘’, alisema Bw. Sendo

Alisisitiza kuwa taarifa za mali zote za umma zilizoko ndani ya taasisi, ziingizwe na kutunzwa kwenye mfumo wa GAMIS na kuondoa hoja ya kutoingiza mali kwenye Mfumo husika na kuhakikisha taarifa hizo zinatumika kwenye kufunga hesabu kwa mwaka 2024/2025 kulingana na Waraka Na. 2 wa Hazina wa mwaka 2021/2022.

Aidha, aliongeza kuwa Maafisa Masuuli wana wajibu wa kuhakikisha kuwa taarifa za ajali, upotevu, hasara za mali za umma zinawasilishwa kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali ndani ya siku 30 mara baada ya tukio kutokea na pia mali iliyopata ajali itafanyiwa matengenezo mara tu baada ya kupata kibali cha matengenezo kutoka kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali.

‘’Sambamba na hilo ni muhimu kuhakikisha kuwa Mali za Miradi zinakabidhiwa kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali (PMG) mara baada ya miradi husika kufikia ukomo pamoja na kusimamia Mali za Umma zinatumika kwa manufaa ya Umma, zinatunzwa na kufanyiwa matengenezo stahiki na kwa wakati’’, alisisitiza Bw.Sendo.

Alisema Serikali imetumia fedha nyingi kuwekeza katika miradi ikiwemo ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere-JNHPP (takribani sh. trilioni 6), ujenzi wa Reli ya kisasa-SGR (takribani sh. trilioni 10.6), ununuzi wa ndege, ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi (takribani sh. bilioni 716.3) pamoja na utekelezaji wa miradi ya maji mijini na vijijini (takribani sh. bilioni 457.4).

Alisisitiza kuwa kutokana na uwekezaji mkubwa na wingi wa rasilimali nchini ni muhimu kuwa na mikakati madhubuti ya kuzisimamia mali hizo ili ziweze kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa na kuiwezesha Serikali kupata manufaa ya uwekezaji uliokusudiwa kwa kipindi kirefu. 

‘’Kwa upande wa Wizara ya Fedha ikiwa na dhamana ya Usimamizi wa Mali za umma nchini imefanya jitihada mbalimbali katika kuongeza ufanisi wa Usimamizi wa Mali za umma nchini kwa Kusimika na kuwezesha matumizi ya mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mali za Serikali “Government Assets Management Information Systems - (GAMIS) ambao unatumika kutunza na kuchakata taarifa za mali za Taasisi zote za Umma hapa nchini’’, alisema Bw. Sendo.

Aidha, Bw. Sendo alisema Wizara imefanya maboresho katika Sheria ya Fedha za Umma sura 348 pamoja na kuandaa Kanuni mahususi za Usimamizi wa Mali za Umma za mwaka 2024 ikiwa ni utekelezaji wa azma ya kuimarisha Mifumo ya Usimamizi wa Mali za Umma nchini.

Alisisitiza Maafisa Masuuli kuwa na mifumo thabiti ya uwajibikaji na kuwa mfano bora kwa wengine kwa kuzingatia misingi ya uadilifu, uwajibikaji, uwazi, na ufanisi katika kuonyesha kwamba mali za umma ni amana ambayo wamekabidhiwa kwa niaba ya Watanzania wote. 

Kwa upande wao mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Makambako, Bi. Appia Clemence Mayemba, aliishukuru Wizara ya Fedha kwa uratibu wa mafunzo hayo, ambapo ameeleza kuwa mada zilizowasilishwa zitawawezesha katika kuboresha utendaji kazi katika halmashauri zao ili kutatua changamoto zinazojitokeza katika usimamizi wa mali za Serikali.

Mafunzo hayo ya siku moja yaliandaliwa na Wizara ya Fedha kwa lengo la kuwajengea uwezo washiriki juu ya Sheria, Kanuni na Miongozo inayohusu masuala ya Usimamizi wa mali za Serikali ili kupunguza hoja za ukaguzi zinazotolewa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG); Wakaguzi wa Ndani pamoja na Wizara ya Fedha kutokana na hakiki zinazotekelezwa na Idara ya Wasimamizi wa Mali za Serikali.

MWISHO.