Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

ESTONIA NA UFARANSA KUISAIDIA TANZANIA KUBORESHA MIFUMO YA KODI NA BANDARI

08 Mar, 2023
ESTONIA NA UFARANSA KUISAIDIA TANZANIA KUBORESHA MIFUMO YA KODI NA BANDARI

Serikali ya Estonia imeahidi kuisaidia Tanzania kuboresha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ya ukusanyaji kodi ili kusaidia kupiga hatua zaidi katika masuala ya usimazi wa kodi na kuongeza uwazi na uwajibikaji.

Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Masuala ya Uchumi na Maendeleo wa Estonia, Mhe. Marjin Ratnik, alipofanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), mjini Doha, Qatar, kando ya Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa nchi zinazoendelea za kipato cha chini unaoendelea nchini humo.

Mhe. Ratnik alisema Serikali yake ipo tayari kuwapokea wataalamu kutoka Tanzania kupata mafunzo ya mifumo ya tehama ya ukusanyaji kodi nchini humo  kwa vitendo ili  wapate utaalam  utakaowasaidia wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Serikali imepokea rasmi mwaliko wa kuwapeleka wataalamu wa Tanzania kupata mafunzo hivyo wameanza maandalizi ya safari hiyo ambapo mwezi Mei mwaka huu wataalam wanaohusika na masuala ya ukusanyaji kodi  watakwenda nchini Estonia kujifunza mifumo mbalimbali ya ukusanyaji kodi.

“Juhudi hizi ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuboresha mifumo ya kodi ili kuwepo na uwazi katika ukusanyaji”, alisema Dkt. Mwigulu.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, alisema kuwa kuwepo kwa mifumo bora ya ukusanyaji kodi itaongeza uwajibikaji wa watalaam wanaohusika na ukusanyaji kodi.

Aliongeza pia kuwepo kwa mifumo ya pamoja ya ukusanyaji kodi itamsaidia mlipakodi kulipa kodi mara moja katika Taasisi zote zinazohitaji kufanya hivyo.

Katika tukio jingine Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa wa Ufaransa, Mhe. Chrysoula Zacharopoulou ambapo Waziri huyo alisema Serikali yake ipo tayari kusaidiana na Tanzania katika ujenzi wa bandari itakayohudumia Tanzania na nchi jirani

“Ufaransa ipo tayari pia kutusaidia kukuza sekta binafsi ambayo imekuwa ikitoa ajira nyingi kwa vijana nchini”, alisema Dkt. Nchemba.

Aliongeza kuwa Serikali ya Ufaransa itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha miundombinu ya barabara, nishati na umeme wa jua ili iweze kutumika katika shughuli za uzajilishaji.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, alisema kuwa  Ufaransa imetangaza rasmi kushirikiana na Tanzania katika kukuza sekta ya utalii  kwa kuwa ina mchango katika pato la Taifa.

Aliongeza kuwa Serikali ya Ufaransa imekuwa ikiisaidia Zanzibar katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo  miundombinu, afya na nishati.

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa wa Ufaransa Mhe. Chrysoula Zacharopoulou, alisema kuwa pamoja na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Ufaransa, anaamini kuwa bado kuna mengi zaidi ya kushirikiana kati ya nchi hizo mbili.

Mhe.  Zacharopoulou alipongeza msimamo wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye masuala ya jinsia na nia ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jukwaa la Usawa wa Kizazi (Generation Equality Forum) baadae mwaka huu.