Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

ELIMU YA FEDHA KUPELEKWA VIJIJINI KWA NJIA YA WASANII

15 Jan, 2024
ELIMU YA FEDHA KUPELEKWA VIJIJINI KWA NJIA YA WASANII

Afisa Msimamizi wa Fedha Mkuu kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, akifungua mafunzo ya elimu ya fedha kwa Wasanii kutoka Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia (TACCI), yanayofanyika mkoani Morogoro, kushoto ni Mkurugenzi wa TACCI, Bi. Aline Augustin na kulia ni mtaalamu wa masuala ya fedha wa Wizara ya Fedha, Bi. Grace Muiyanza.

 

Wananchi wametakiwa kukopa kwenye taasisi za fedha zilizosajiliwa na kutambulika na Benki Kuu ya Tanzania au Mamlaka Kasimishwa kwa kuwa itasaidia kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza kwa mkopaji kwa kuwa taasisi hizo zinaendeshwa kwa mujibu wa Sheria.

Rai hiyo imetolewa mkoani Morogoro na Afisa Msimamizi wa Fedha Mkuu kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, wakati akifungua Mafunzo ya Elimu ya Fedha kwa Wasanii kutoka Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia (TACCI)

Alisema kuwa mkopaji anapaswa kuwa na elimu sahihi kuhusu huduma za fedha

na kusoma na kuelewa vyema mikataba ya mikopo ili kufahamu gharama halisi za mkopo na kuziafiki kabla ya kuchukua husika mkopo ili kuepuka kuingia hasara kwa kudhulumiwa.

“Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha, umeelekeza kutoa elimu ya fedha kwa umma kwa njia mbalimbali, hivyo mafunzo kwa wasanii yatawezesha kupeleka elimu ya fedha vijijini ambako kumekuwa na uelewa mdogo wa masuala hayo na kusababisha uwepo na mikopo umiza”, alisema Kimaro

Alisema kuwa mwananchi anapokopa ni lazima ajue riba, ada na gharama zingine lakini pia mkopaji anapaswa kujua kiasi ambacho anatakiwa kulipa kwa kipindi chote cha mkopo.

Alisema kuwa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ni Mpango uliowekwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha katika kuhakikisha huduma za fedha zinaimarika, mitaji inapatikana na kunakuwa na Sekta ya fedha himlivu inayochangia ipasavyo kwenye pato la Taifa.

Bw. Kimaro, alisema kuwa program ya elimu kwa umma inatekelezwa kwa kipindi cha miaka 5 kuanzia 2020/2021 hadi 2025/2026 ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa miaka 10 kuanzia 2020/2021 hadi 2029/2030.

Alieleza kuwa baada ya hapo Mpango Mkuu utafanyiwa tathmini ili kuona mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wake na kuja na maboresho iwapo changamoto zitajitoeza.

Bw. Kimaro, alisema kuwa Sanaa ni eneo muhimu la kufikisha ujumbe kwa umma kwa kuwa ni rahisi kuwafikia wananchi na njia yenye mafanikio makubwa si tu kwa Tanzania lakini pia duniani kwa ujumla.

Alibainisha kuwa maeneo muhimu ambayo yataangaziwa wakati wa kutoa elimu ya fedha ni pamoja na usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji wa akiba, mikopo, uwekezaji, bima, bima ya amana, mpango wa kujiandaa na maisha ya uzeeni, kodi, mifumo ya malipo na kuwalinda watumiaji wa huduma za fedha

“Tutaenda vijijini na tutachagua maeneo ambayo elimu ya fedha ipo chini baada ya wasanii kupata uelewa ili kupeleka elimu sahii kwa wananchi”, aliongeza Bw. Kimaro.

Aidha, alisema kuwa mkopaji anashauriwa kukopa kwa ajili ya uwekezaji unaozalisha kama vile kununua sehemu ya ardhi ambapo ataweza kuzalisha mazao au kupanua biashara itakayomwezesha mkopaji kurejesha mkopo kwa wakati na kuweza kukopa zaidi baadae kama atahitaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia (TACCI), Bi. Aline Augustin, alisema kuwa upekee katika kuelimisha jamii ni matumizi ya Sanaa za maonesho jukwaani kwa ajili ya maendeleo ya jamii, kwa kutumia pia ngoma bila maneno na maigizo kwa njia ya redio.

‘’Kwa njia ya redio na ngoma TACCI, inakuwa na nafasi kubwa ya kuifikia jamii na kupenyeza elimu na kuvutia watu wa makundi tofauti kwa kuwaleta pamoja na kuchochea mazungumzo na majadiliano katika elimu inayotolewa’’, alisema Bi. Augustin

Aidha, alisema kuwa mafunzo ya elimu ya fedha yanayoendelea kutolewa yanawapa uelewa na wigo mpana wa kuandaa elimu kwa njia ya sanaa itakayokidhi matakwa ya Wizara ya Fedha katika kufikisha ujumbe stahiki kwa wananchi hususani waishio vijijini.

Bi. Augustine, ameipongeza Wizara ya Fedha kwa kuamua kutumia sanaa kufikisha elimu vijijini na ameahidi kutumia mafunzo wanayopata kuongeza ujuzi na kuhakikisha elimu ya fedha kwa njia ya sanaa inawasilishwa kwa ufanisi na kwa tija.

Mwisho.