Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

DKT. NCHEMBA ATETA NA VIONGOZI WA MIKOA TANZANIA BARA

28 Aug, 2023
DKT. NCHEMBA ATETA NA VIONGOZI WA MIKOA TANZANIA BARA
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akitoa mada ya hali ya uchumi na utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2023/2024, katika mkutano wa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa iliyoandaliwa na TAMISEMI katika Shule ya Uongozi ya Julius Nyerere-Kibaha mkoani Pwani, na kuwataka Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kusimamia ipasavyo makusanyo ya mapato ya ndani pamoja na kulinda biashara ili kuiwezesha Serikali kupata mapato yatakayofanikisha kutekeleza miradi yake inayolenga kuchochea maendeleo ya nchi pamoja na kuimarisha sekta za uzalishaji na kukuza ajira.
 
 
 
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewataka Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kusimamia ipasavyo shughuli za biashara katika maeneo yao na kuwazuia watendaji wa Taasisi za Serikali kufunga biashara za watu kunapojitokeza mizozo ya ukusanyaji kodi, tozo na mambo mengine kwa sababu hatua za kufunga biashara na ofisi hizo ina athari kubwa kiuchumi na ajira za watu
 
Dkt. Nchemba alitoa rai hiyo Katika Shule ya Uongozi ya Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani, wakati akitoa mada kuhusu hali ya uchumi wa nchi na utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara, ulioandaliwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI.
 
Dkt. Nchemba alirejea rai yake kwa watendaji wa Serikali kuacha kufunga biashara za watu kunapotokea ukiukwaji wowote wa sheria za ukusanyaji wa kodi, ada na tozo kwani ufungaji wa biashara au kutoza faini kubwa kwa sababu zozote zile una athari kubwa za kiuchumi na kuathiri ajira za wananchi, mapato ya kampuni na mapato ya Serikali.
 
“utaratibu huu unakwenda kinyume na juhudi kubwa za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini, nilielekeza na naendelea kusisitiza kuwa ni marufuku kwa taasisi yoyote ya Serikali kufunga biashara, ofisi ama maeneo yoyote ya uzalishaji kwa kigezo cha kukiuka taratibu mbalimbali bali mwenye biashara achukuliwe hatua kwa makosa ya biashara na siyo kuifunga biashara yenyewe” Alisisitiza Dkt. Nchemba
 
Usimamizi wa makusanyo ya mapato na matumizi ya Serikali
 
Aidha, Mhe. Dkt. Nchemba aliwahimiza viongozi hao wa mikoa kuweka usimamizi madhubuti wa ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za umma katika maeneo wanayoyasimamia ili kufikia malengo na kuwezesha juhudi za Serikali katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na ujenzi wa miundombinu wezeshi kwa ajili ya utoaji wa huduma za msingi za kijamii ikiwemo elimu, afya na maji safi na salama
 
Alisema kuwa katika mwaka wa Fedha wa 2023/24, Serikali inatarajia kukusanya jumla ya shilingi trilioni 44.39 kutoka kwenye vyanzo vyote ambapo kati ya kiasi hicho, mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Halmashauri yanatarajiwa kuchangia asilimia 70.7, misaada na mikopo nafuu asilimia 12.3 na mikopo ya kibiashara kutoka ndani na nje ya nchi asilimia 17.0
 
Alihimiza mifumo ya TEHAMA itumike kikamilifu katika ukusanyaji wa mapato na kudhibiti vitendo vya ukwepaji kodi hasa maeneo ya mipakani ambapo biashara haramu na magendo hufanyika kwa wingi na hivyo, kuikosesha Serikali kodi stahiki.
 
Ushiriki wa Sekta Binafsi katika shughuli za Maendeleo
 
Mhe. Dkt. Nchemba alitoa pia rai pia kwa Wakuu hao wa Mikoa na Makatibu Tawala wao kuishirikisha kikamilifu sekta binafsi kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao kupitia utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) pamoja na kuhakikisha miradi inayoibuliwa na kutekelezwa inakuwa na tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla kwa kukagua thamani ya fedha iliyotumika pamoja na viwango vinavyotakiwa.
 
Alisema kuwa Serikali imeendelea kuhakikisha kunakuwepo na mazingira wezeshi kwa ajili ya kuchochea ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo kuboresha mifumo wa kisheria ambapo Juni 2023 Serikali ilikamilisha mapitio ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi, Sura 103 na yaliridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
“Lengo ni kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa utaratibu wa PPP ambapo utaratibu huu unatumika kama njia mbadala ya kugharamia miradi iliyopaswa kutekelezwa na Serikali na hivyo kupunguza mzigo katika bajeti na kuchochea maendeleo.” Alisema Dkt. Nchemba
 
Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma
 
Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alibainisha kuwa takribani asilimia 70 ya bajeti ya Serikali hutumika katika ununuzi wa umma na huku ndiko kwenye mianya mikubwa ya upigaji fedha za umma. 
 
Alisema kuwa Serikali imeshakamilisha mapitio ya Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410 na inatarajiwa kusomwa bungeni katika Bunge linalotarajiwa kuanza Agosti 29, 2023. 
 
“Sambamba na hilo, tunakamilisha ujenzi wa mfumo mpya wa kielektroniki wa ununuzi (NeST) kwa kutumia wataalamu wa ndani ambapo lengo la maboresho hayo ni kuufanya mfumo wa ununuzi wa umma kuwa wa kimkakati pamoja na kuziba mianya ya ubadhirifu kwa lengo la kupata thamani ya fedha katika matumizi ya Serikali. 
 
Baadhi ya Wakuu wa mikoa walisema kuwa masuala yaliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, katika mkutano huo yamebeba agenda za kitaifa na yanahusu maendeleo ya nchi na kuahidi kwenda kuyasimamia kama maelekezo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
 
Mwisho