Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

DKT. NCHEMBA AITAKA TIA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE KIKAMILIFU CHINI YA MRADI WA HEET

05 Jan, 2024
DKT. NCHEMBA AITAKA TIA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE KIKAMILIFU CHINI YA MRADI WA HEET

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameitaka Kamati ya ushauri wa kitasnia ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) chini ya mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi kwa Vyuo vya Elimu ya Juu nchini (HEET) kutekeleza majukumu yake kikamilifu ili kubaini, kushauri na kupendekeza mwelekeo wa mahitaji ya viwanda nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Mhe. Waziri wa Fedha wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa kitasnia chini ya mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi kwa Vyuo vya Elimu ya Juu jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, alisema kamati hiyo itakuwa na mchango mkubwa katika uhuishaji na uandaaji wa mitaala itakayokidhi soko la ajira na kujua mahitaji halisi za sekta ya viwanda.

“Ni matarajio yangu kuwa Kamati hii itatoa ushauri muhimu kwa Taasisi katika masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa programu mpya zenye kukidhi soko la ajira na zenye kumuandaa mhitumu kujiajiri na zitakazochochea ushirikiano kwenye maeneo ya utafiti na ushauri wa kitaalamu, pamoja na mafunzo ya vitendo kwa Wanachuo na Wahadhiri,” alisema Bi. Amina Khamis Shabaan.

Bi. Shaaban alisema Kamati hiyo itakuwa kiunganishi kati ya idara za taaluma na viwanda mbalimbali kupitia miongozo na ushauri elekezi utakaokuwa unatolewa na itakuwa kiungo muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya Taasisi na wadau wake ambao ni sekta binafsi na Umma.

Alisema kuwa Taasisi za elimu ya juu duniani hususan nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania zinakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya kusomea na kufundishia hususan ile ya kidigitali, uhaba wa wahadhiri wa ngazi mbalimbali, mitaala isiyoendana na uhalisia wa soko la ajira hivyo ni vema changamoto hizo zikatafutiwa majibu.

Alisema kamati ya Ushauri wa Kitasnia ni dhana inayojulikana kote mfano Ulaya, Asia na Afrika, na kwamba inalenga mahusiano kati ya Taasisi za Elimu ya Juu na Viwanda.

Alisema kwa kutambua hilo Serikali iliamua kutumia mradi huo kuyarasimisha na kuhakikisha misingi madhubuti inawekwa ili taasisi za elimu ya juu zishirikiane na wadau wengine kwa pamoja kuhakikisha vyuo vyote vinapata nafasi ya kujua waajiri wanahitaji ujuzi wa aina gani.

Aidha aliitaka kamati hiyo kujifunza kutoka nchi mbalimbali zilizofanikiwa kwa kuona fahari juu ya elimu yao na kuhakikisha kuwa viwanda vilivyopo nchini vinalindwa na kutatua tatizo la soko la ajira.

Naye Mtendaji Mkuu wa Chuo cha TIA, Prof. William Pallangyo, alisema taasisi yake kupitia mradi wa HEET pamoja na utekelezaji wa mambo mbalimbali imeweza kugharamia kazi ya Ushauri wa tathmini ya athari kwa Mazingira na Kijamii (ESIA) kwa majengo ya Taaluma katika Kampasi ya Singida na mabweni mawili katika Kampasi ya Mwanza na kununua vifaa vya TEHAMA.

Vilevile maeneo mengine ni pamoja na kujenga uwezo kwa viongozi wakuu sita, Wahadhiri watatu Wanawake kwenda kwenye mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya Shahada ya Uzamivu

Aidha Prof. Pallangyo alisema kuwa TIA ni miongoni mwa Taasisi za Elimu ya Juu chini ya Wizara ya Fedha, zinazoshiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Mradi wa HEET ambapo imetengewa jumla ya Dola za Marekani milioni 11.768 sawa na shilingi za kitanzania bilioni 27.6.

Mradi wa HEET ni matokeo ya mkopo wa dola milioni 425 wenye masharti nafuu sana kutoka Benki ya Dunia.

MWISHO