Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

DKT. NCHEMBA AIOMBA BENKI YA DUNIA KUISAIDIA SERIKALI KUKABILIANA NA UPUNGUFU WA DOLA ZA MAREKANI

06 Sep, 2023
DKT. NCHEMBA AIOMBA BENKI YA DUNIA KUISAIDIA SERIKALI KUKABILIANA NA UPUNGUFU WA DOLA ZA MAREKANI
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (katikati-mbele), akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Benki ya Dunia ukiongozwa na Mkurugenzi wake anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bw. Hassan Zaman (wa pili kulia), baada ya kukutana na kufanya mazungumzo katika Ofisi za Hazina Ndogo Jijini Dar es Salaam, ambapo wamejadili masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Benki hiyo, ikiwemo namna ya kuisadia nchi kukabiliana na athari za upungufu wa dola za Marekani katika mzunguko wa fedha, ili kulinda ukuaji wa uchumi, na umuhimu wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa nchi. Kulia ni Meneja Uendeshaji wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, Bi. Preeti Arora, akifuatiwa na Meneja Mkazi wa Benki ya Dunia Bw. Nathan Belete.
 
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameiambia Benki ya Dunia kwamba Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kuiwezesha sekta binafsi kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi na kuwezesha upatikanaji wa fedha za kigeni kupitia uwekezaji wa mitaji kutoka ndani na nje ya nchi.
 
Dkt. Nchemba, amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Benki ya Dunia, ukiongozwa na Mkurugenzi anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bw. Hassan Zaman, katika Ofisi za Hazina Ndogo Jijini Dar es Salaam.
 
Katika mkutano huo  wamejadili masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Benki hiyo, ikiwemo namna ya kuisadia nchi kukabiliana na athari za upungufu wa dola za Marekani katika mzunguko wa fedha, ili kulinda ukuaji wa uchumi.
 
Alisema kuwa Serikali kupitia Bunge, limepitisha mabadiliko mbalimbali ya sheria na kanuni zitakazowezesha kuvutia uwekeaji wa mitaji na teknolojia ambapo sheria kadhaa zimefanyiwa marekebisho na sheria nyingine ya masuala ya ununuzi wa umma itajadiliwa bungeni ambapo maboresho ya sheria hiyo yatachochea zaidi uwekezaji.
 
Aliiomba pia Benki hiyo kuharakisha upatikanaji wa zaidi ya dola za Marekani Milioni 500 ifikapo mwezi Novemba mwaka huu ili fedha hizo zisaidie nchi kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa dola za Marekani katika mzunguko wa fedha nchini hali inayochangia mfumuko wa bei na kukwamisha uagizaji wa bidhaa muhimu kutoka nje ya nchi ikiwemo mafuta.
 
Aidha, Dkt. Nchemba aliishukuru Benki ya Dunia kwa kuidhinisha upatikanaji wa fedha kwenye miradi 8 yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 2.16 kati ya miradi 26 yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 5 ambayo Serikali imewasilisha kwenye Benki hiyo, na kwamba miradi hiyo itakapokamilika itakuwa na matokeo chanya katika kukuza uchumi na maendeleo ya watu.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bw. Hassan Zaman, alipongeza jitihada kubwa zilizofanywa na Tanzania katika kusimamia na kukuza uchumi wake licha ya uwepo wa changamoto za athari za UVIKO 19 na vita baina ya Urusi na Ukraine na kwamba nchi nyingi za Afrika zinapaswa kujifunza kutoka Tanzania kuhusu usimamizi wa sera za fedha na uchumi.
 
Alipongeza pia hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini ambapo amesisitiza kuwa hatua hizo zitawavutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza katika sekta muhimu za uzalishaji na hivyo kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.
 
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Meneja Mkazi wa Benki ya Dunia Bw. Nathan Belete, Meneja Uendeshaji anayesimamia nchi za Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, Bi. Preeti Arora, Kamishna wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade na maafisa wengine kutoka Tanzania na Benki ya Dunia.
 
Mwisho.