Category Title

  • Government Budget Speeches
  • Ministry's Budget Speeches
  • Budget Books 2024/2025
  • Budget Books 2023/2024
  • Budget Books 2022/2023
  • Budget Books 2021/2022
  • Budget Books 2020
  • Budget Books 2018/2019
  • Budget Books 2015/2016
  • Budget Books 2014/2015
  • Content not found
  • Content not found
  • Content not found

BENKI YA AfDB YAONESHA NIA KUONGEZA NGUVU UTEKELEZAJI WA MRADI WA SGR

05 Jul, 2023
BENKI YA AfDB YAONESHA NIA KUONGEZA NGUVU UTEKELEZAJI WA MRADI WA SGR

Na Peter Haule, WFM, Dodoma

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) pamoja na mambo mengine imeonesha nia ya kuongeza nguvu katika kusaidia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR)

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alipo kutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayeshughulikia Sekta ya Kilimo na Maendeleo ya kibinadamu na kijamii, Bi. Beth Dunford.

Alisema kuwa AfDB imeonesha nia ya  ushiriki kwenye  mradi mkubwa wa kimkakati wa Reli ya Kisasa (SGR) kwenye baadhi ya maeneo ambayo hayajakamilika.

Vilevile Benki hiyo imeonesha nia ya kushirikiana na Serikali kuongeza mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) ambayo ni chachu ya utekelezaji wa miradi ya kilimo kwa upande wa umwagiliaji na uongezaji wa thamani.

Alisema maeneo mengine ambayo yamejadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na Miradi ya maeneo mahususi ya kilimo na kukuza ushiriki wa vijana katika shughuli za uzalishaji, mradi wa maeneo mahususi ya kilimo na mifugo.

Kuhusu wazo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan la kuanzishwa Benki ya Vijana, Dkt. Nchemba alisema kuwa wamekubaliana timu ya wataalamu kukutana ili kuangalia namna jambo hilo linavyoweza kutekelezwa

Dkt. Nchemba ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kwa niaba ya Serikali ya Tanzania kwa msaada walioutoa katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo ya miundombinu, nishati, kilimo, maji na elimu.

Amesema kuwa kiasi cha takribani dola za Marekani bilioni 2.6 kimetolewa na benki hiyo kwa ajili ya kutekeleza miradi 24, ambapo sekta ya kilimo imepewa asilimia nne ya fedha zote ambazo zimeletwa nchini kupitia Benki hiyo ambapo zinaboresha uzalishaji ikiwa ni pamoja na kukuza kilimo cha mazao kama ngano, alizeti na kuongeza kipato kwa mkulima.

Aidha alieleza kuwa nchi za Afrika zilikubaliana kuongeza uwekezaji kwenye kilimo cha umwagiliaji, kuongeza thamani ya bidhaa na mazingira bora ya uhifadhi wa bidhaa jambo ambalo Serikali inalitekeleza kwa kuongeza bajeti kwenye sekta ya kilimo.

Alisema kuwa Serikali imeongeza bajeti kutoka shilingi bilioni 294 kwa mwaka 2021/20222 hadi shilingi bilioni 970.8 kwa mwaka 2023/2024.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayeshughulikia Sekta ya Kilimo na Maendeleo ya kibinadamu na kijamii, Bi. Beth Dunford, ameipongeza Serikali kwa juhudi zake za maendeleo na kuahidi kuwa AfDB itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kufanikisha miradi mbalimbali ikiwemo   miradi ya uzalishaji kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Mkutano huo ulioongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Nchemba, umewashirikisha pia Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) pamoja na Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu wa Wizara hizo.

Mwisho.