WIZARA YA FEDHA YAANZA KUTOA ELIMU YA FEDHA KUPITIA SANAA

Wizara ya Fedha kupitia Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji Elimu ya Uraia (TACCI) wamefanikiwa kuwafikishia elimu ya Fedha baadhi ya wakazi wa Morogoro kwa njia ya Sanaa ikiwa ni mwanzo wa mkakati wa kufikisha elimu hiyo nchi zima ili kutekeleza Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kwaka 2021/2022 hadi 2029/2030. Akizungumza baada ya elimu hiyo iliyotolewa mtaa wa Malikula Chamwino, mkoani Morogoro, Afisa Msimamizi wa Fedha Mkuu kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, alisema kuwa elimu kwa njia ya Sanaa mkoani Morogoro ni mwanzo wa matukio kama hayo yatakayofanyika nchi nzima hususan maeneo ya vijijini kwa kuwa njia hiyo imeonesha mafanikio makubwa.