WAZIRI WA FEDHA AZINDUA HARAMBEE, AWATAKA WANANCHI KUENZI MCHANGO WA MASHEIKH WALIOTANGULIA MBELE YA HAKI
Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amewataka waumini wa dini ya kiislam kuendelea kuenzi mchango wa viongozi wa dini waliotangulia mbele ya haki kwa kudumisha maadili, mshikamano na amani katika jamii.
Waziri Balozi Omar alitoa wito huo alipokuwa Mgeni Rasmi katika dua na harambee ya kuwaombea Masheikh waliotangulia mbele ya haki iliyofanyika Buguruni Malapa, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi wa dini, Serikali na wananchi wa Buguruni, Mhe. Balozi Omar alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha washiriki kukutana katika mkusanyiko huo wa kheri wa kuwaombea Masheikh, wazazi na ndugu waliotangulia mbele ya haki.
