TANZANIA YANG’ARA KIMATAIFA KWA USIMAMIZI BORA WA DENI LA SERIKALI

Serikali ya Tanzania imeendelea kung’ara katika jukwaa la kimataifa baada ya kuibuka mshindi wa jumla wa mwaka katika Tuzo za Usimamizi wa Deni la Umma za Jumuiya ya Madola na tuzo ya Ofisi Bora Kanda ya Afrika kupitia Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha (Debt Management Division), ambazo zilitangazwa tarehe 26 Machi 2026 wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Jumuiya ya Madola kuhusu Usimamizi wa Deni la Umma, uliofanyika jijini London, nchini Uingereza. Ushindi huo mkubwa unatokana na juhudi za Serikali katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa deni la umma, ikiwemo kuunganisha vyema mifumo ya kifedha ya Serikali na kuboresha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya maendeleo, ambapo Jopo huru la wataalamu lililochambua mawasilisho kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Madola lilizingatia vigezo vya ubunifu, uimara na uendelevu katika kutoa tuzo hizo.