TANZANIA YAJIPANGA KUONGEZA UFANISI UKUSANYAJI WA MAPATO

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban amesema kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Jumuiya ya Madola, katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa rasilimali za ndani kupitia mifumo ya kisasa ya ukusanyaji kodi na ukaguzi wa forodha (IDRAS na TANCIS), pamoja na utekelezaji wa Mkakati wa Kipindi cha Kati wa Mapato. Bi. Amina amesema hayo wakati akimwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba katika kikao cha Jukwaa la Kimataifa linalowakutanisha Mawaziri wa Fedha kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, (Commonwealth Finance Ministers Meeting, CFMM 2025), kilichofanyika kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia, Jijini Washington D.C, nchini Marekani.