TANZANIA YADHAMIRIA KUIMARISHA BIASHARA NA UWEKEZAJI KUPITIA USHIRIKIANO NA ATIDI.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha zaidi ushirikiano na Shirika la Bima ya Maendeleo ya Biashara na Uwekezaji Afrika (ATIDI) katika juhudi za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, sambamba na kuvutia mitaji zaidi ya sekta binafsi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika Warsha ya ATIDI kuhusu “Kuimarisha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Tanzania” iliyofanyika hoteli ya Hyatt Regency, Mhe. Balozi Omar alilisifu shirika hilo kwa mchango wake mkubwa katika kutoa huduma za kupunguza hatari za uwekezaji (de-risking), hatua inayowapa wawekezaji na taasisi za kifedha ujasiri wa kushiriki katika miradi mikubwa barani Afrika.
