TANZANIA, AFREXIMBANK ZAJADILI SGR, AMCE NA UAGIZAJI WA MAFUTA

Benki ya Afrika ya Uagizaji na Usafirishaji Nje ya Nchi (African Export-Import Bank-Afreximbank) imesema iko tayari kuendelea kuisaidia Tanzania kupata fedha za ujenzi wa Reli ya Kisasa-SGR pamoja na kuwekeza kwenye miradi mipya ya sekta ya madini na ujenzi wa mradi mkubwa wa hospitali itakayokuwa na viwango vya dunia vya utoaji huduma za matibabu (African Medical Center of Excellence (AMCE). Ahadi hiyo imetolewa Jijini Washington D.C, nchini Marekani na Makamu wa Rais wa Afriexim Bank (Global Trade Bank), Bw. Haytham ElMaayergi, alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), pembezoni mwa Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF.