SERIKALI NA IFC YAANZA KUPITIA MIRADI YA KIMKAKATI YA PPP

NAIBU Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jenifa Omolo, amesema kuwa Serikali imeifanyia marekebisho sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ili kuvutia uwekezaji wa mitaji yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 9 sawa na shilingi trilioni 21.03 kutoka Sekta Binafsi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Bi. Omolo alisema hayo Jijini Dar es Salaam, wakati akifungua kikaokazi kati ya Mamlaka 8 za Serikali na Shirika la Kimataifa chini ya Benki ya Dunia, linalohusika na kutoa mikopo na misaada ya kiufundi kwa sekta binafsi, (International Finance Corporation-IFC), kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu Mwamba.