MAAFISA MASUULI WATAKIWA KUONDOSHA MALI CHAKAVU KUFIKIA SEPTEMBA 2025.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, ameagiza Maafisa Masuuli nchini kuhakikisha kuwa mali zote za umma ambazo ni chakavu, sinzia na ziada na zilizokwisha matumizi zinaondoshwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo kufikia tarehe 30 Septemba, 2025.
Maagizo hayo yametolewa kwa niaba yake mkoani Njombe, na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Chotto Sendo, wakati akifungua Mafunzo ya Usimamizi wa Mali za Umma kwa Maafisa Masuuli.
Bw. Sendo alisema kuwa kuelekea kuanza rasmi mwezi wa kwanza wa mwaka wa fedha 2025/2026, Maafisa Masuuli kwa kushirikiana na Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali ni vema kuzingatia kuwa mali zilizokwisha matumizi zinaondolewa kwa wakati.