LWANGILI AIPONGEZA WIZARA YA FEDHA KWA KUTUMIA CAPITAL CITY MARATHON KUFIKISHA ELIMU YA FEDHA KWA WANANCHI
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Prisca Lwangili, ameipongeza Wizara ya Fedha kwa kutumia mbio za Capital City Marathon (CaCiMa) kama jukwaa la kuwafikishia wananchi elimu ya fedha, akieleza kuwa majukwaa ya aina hiyo yana nafasi muhimu katika kuwafikia watu wa makundi mbalimbali na kuwajengea uwezo wa kusimamia rasilimali zao.
Bi. Lwangili ametoa kauli hiyo wakati wa mbio hizo zilizofanyika katika Viwanja vya Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), jijini Dodoma, kuanzia Oktoba 31 hadi Novemba 1, 2026, ambapo Wizara ya Fedha ilishiriki kwa kutoa elimu kupitia wataalamu wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha na Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali.
