IMF YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA KUKUZA UCHUMI NA HUDUMA ZA JAMII

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amefunga vikao vya majadiliano kati ya Serikali na Timu ya Wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) baada ya kukamilisha tathimini ya utekelezaji wa program ya Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuchachua uchumi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii. Akifunga vikao hivyo katika Kikao cha majumuisho kilichofanyika Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam, Dkt. Nchemba, alieleza kufurahishwa kwake na taarifa ya awali ya Timu hiyo iliyowasilishwa na Kiongozi wa Timu hiyo Bw. Harris Charambos Tsangarides, inayoonesha kuwa Tanzania imetekeleza ipasavyo vigezo vilivyowekwa na Shirika hilo la Fedha la Kimataifa IMF na kwamba itaendelea kusimamia ipasavyo program hiyo yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 1.1 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 2.4, ambayo itatekelezwa katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu.