DKT. NCHEMBA AONGOZA MKUTANO WA WB KANDA YA AFRIKA

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameongoza mkutano wa Benki ya Dunia wa Jukwaa la Tatu la Kanda ya Afrika Kundi la Kwanza kwa nchi za Kipato cha Kati uliolenga kujadili namna mashirika ya fedha ya kimataifa yanavyoweza kuongeza fedha kwa ajili ya kuzisaidia nchi za kipato cha kati ili ziweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika nchi zao itakayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii. Akifungua mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Mkutano huo, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema kuwa Dunia inakabiliwa na migogoro mingi na changamoto za maendeleo ya kiuchumi ambazo zinasababisha kutofikiwa kikamilifu kwa malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).