DKT. MWIGULU AKIPONGEZA CHUO CHA MIPANGO KWA KUWAINUA WANANCHI KIUCHUMI.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amekipongeza Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) kwa kuwainua wananchi kiuchumi kupitia Kituo cha Ujasiriamali na Ubunifu cha Chuo hicho (Mipango Enterprenurship and Innovation Centre - MEI), pamoja na miradi inayoendeshwa na wabia wa maendeleo wakiwemo Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Akizungumza kwa niaba ya Mhe. Waziri wa Fedha katika mahafali ya 37 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini duru ya kwanza Kampasi Kuu – Dodoma, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo, amekitaka Chuo hicho kuendelea kutilia mkazo mawazo ya kijasiriamali na ubunifu ya wanafunzi kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwawezesha vijana kushiriki kwenye mapinduzi makubwa ya kiuchumi.