BENKI YA DUNIA YAIPONGEZA TANZANIA KUWEKEZA KWENYE KILIMO

Benki ya Dunia imeipongeza Tanzania kwa kuamua kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye maeneo ya uzalishaji kikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi mambo ambayo yatachochea ukuaji wa kipato cha wananchi na kukuza uchumi wa nchi. Pongezi hizo zimetolewa Jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Kusini Mashariki, Bi. Victoria Kwakwa, alipokutana na kufanya mazungumzo rasmi na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba. Aliahidi kuwa Benki yake na washirika wake wengine watasaidia juhudi za Serikali za kufanikisha mapinduzi katika sekta hizo muhimu kwa kutoa fedha pamoja na ushauri wa kitaalam ili mpango huo wa kuendeleza kilimo, mifugo na uvuvi uwe na tija.