BENKI YA DUNIA YAAHIDI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA TANZANIA

MAKAMU Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, ameahidi kuwa Benki yake itaendelea kuiunga mkono Tanzania katika kufanikisha malengo yake ya kukuza uchumi na kuwahudumia wananchi wake huku akipongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kusimamia uchumi wake. Bi. Kwakwa ametoa pongezi hizo Jijini Washington D.C nchini Marekani, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania, ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, kwenye mikutano ya kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF.