BENKI YA DUNIA WAENDELEA KUIFAGILIA TANZANIA KWA KUSIMAMIA UCHUMI

BENKI ya Dunia imeendelea kuimwagia sifa Tanzania kwa usimamizi mzuri na mageuzi makubwa ya kiuchumi ikilinganishwa na nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara katika kipindi ambacho Dunia inahangaika na misukosuko inayotokana na athari za UVIKO 19, mizozo ya vita pamoja na kuyumba kwa soko la fedha za kigeni. Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo anayesimamia Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency), Dkt. Floribert Ngaruko, walipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), inayofanyika Jijini Marrakech, nchini Morocco.