BENKI YA DUNIA, TANZANIA, BUNRUNDI WAJADILI USHIRIKIANO WA KIUCHUMI KATIKA USHOROBA WA KATI.

Mawaziri wa Fedha wa Tanzania na Burundi, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar na Mhe. Dkt. Alain Ndikumana, kwa pamoja, wamekutana na wawakilishi wa Benki ya Dunia wakiongozwa na Makamu wa Rais anayehusika na Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop, kujadili namna ya kuharakisha utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa miundombinu wa Ushoroba wa Kati (Central Corridor), unaolenga kubadilisha mtandao wa usafirishaji wa kikanda kuwa kichocheo muhimu cha ustawi wa kiuchumi katika ukanda huo. Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Omar amesema kuwa majadiliano hayo yalilenga kuubadilisha Ushoroba wa Kati kutoka kuwa njia ya kawaida ya usafirishaji na kuwa eneo jumuishi la kiuchumi huku msisitizo mkubwa ukiwekwa katika maendeleo ya Reli ya Kisasa (SGR) ikiunganishwa na miundombinu ya bandari ya Dar es Salaam, sambamba na uwekezaji katika sekta za kilimo, madini na viwanda.