BENKI YA DUNIA KUSAIDIA TANZANIA KUWEKEZA KWENYE NISHATI NA SGR
BENKI ya Dunia imeahidi kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa nishati ya umeme itakayotumiwa na nchi za Afrika ili kulinda usalama wa kiuchumi na uzalishaji wa bidhaa katika kipindi kifupi kijacho pamoja na kuongeza thamani ya mradi wa treni iendayo kasi (SGR) ili iweze kuwanufaisha wananchi na wawawekezaji katika korido ambayo miundombinu ya treni itapita.
Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiamé Diop, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania, unaoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, kwenye Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, inayofanyika Jijini Washington D.C, nchini Marekani.