BARA LA AFRIKA LIWEKE MIKAKATI YA KUKABILIANA NA ATHARI ZA VITA MASHARIKI YA KATI

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, ametoa wito kwa nchi za Afrika kuwa na mtazamo wa pamoja katika kubuni na kutekeleza mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu, ambayo ni endelevu na jumuishi, itakayopunguza utegemezi na kuimarisha uthabiti wa uchumi wa Bara la Afrika ili kukabiliana na majanga na migogoro ya vita inayoendelea duniani. Mhe. Balozi Omar alitoa wito huo jijini Tangier nchini Morocco, katika Mkutano wa 58 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi na Magavana wa Benki Kuu wa Afrika, wakati akichangia mjadala kufuatia taarifa ya Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayosimamia Uchumi Afrika (UNECA), inayochambua athari za mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati namna ulivyoleta athari hasi za kiuchumi na kijamii katika Bara la Afrika.