WIZARA YA FEDHA YAANZA MCHAKATO WA KUANZISHA SHERIA YA UKAGUZI WA NDANI.
Wizara ya Fedha, imeanza mchakato wa kuanzisha Sheria Maalum ya Ukaguzi wa Ndani ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa udhibiti wa ndani na kuweka msingi imara wa kisheria na kitaasisi kwa shughuli za ukaguzi nchini.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), kupitia Hotuba yake iliyosomwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), alipomwakilisha katika Mkutano wa 19 wa Mwaka wa Ukaguzi wa Ndani pamoja na Jukwaa la 13 la Utawala Bora, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), ulioandaliwa na Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani Tanzania (The Institute of Internal Auditors- Tanzania).
