WATOA HUDUMA NDOGO ZA FEDHA WATAKIWA KUWAPA MIKATABA WANANCHI WANAOWAKOPESHA
Watoa huduma ndogo za fedha na vikundi vya kijamii nchini vinavyojihusisha na huduma za mikopo vimetakiwa kuwapatia nakala ya mkataba wananchi wanaowakopesha mikopo.
Akizungumza katika program ya elimu ya fedha kwa wananchi wa Mji Mdogo wa Mikumi, Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bi. Grace Muiyanza, alisema kuwa watoa huduma wanatakiwa kutoa mikataba kwa wanaowakopesha kwa mujibu wa sheria iliyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.