WASTAAFU WANAOLIPWA NA HAZINA WAASWA KUEPUKA MATAPELI

Wizara ya Fedha imeawaasa wastaafu wanaolipwa mafao na Hazina kujiepusha na jumbe kwa njia ya simu zinazotumwa na watu wasiojulikana zikiwaelekeza kutuma fedha ili kuhakikiwa kwani wanaweza kutapeliwa fedha zao na matapeli hao. Akizungumza wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma, Afisa Hesabu Mkuu, Kitengo cha Pensheni Wizara ya Fedha Bi. Joyce Chacky, alisema kuwa hakuna zoezi la uhakiki wa wastaafu linalofanywa na Hazina pia hakuna zoezi la uboreshwaji wa pensheni kwa mstaafu mmoja mmoja.