WANANCHI WAASWA KUTUMIA NAMBA YA MALIPO WANAPOLIPIA HUDUMA ZA SERIKALI

Wananchi wametakiwa kutumia Namba ya malipo (Control Number) kila wanapofanya malipo ya Serikali ili kuwa na uhakika wa malipo waliyofanya yanafika mahali sahihi kwa ajili ya kutumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo zikiwemo za ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu na maji. Hayo yamesemwa na Afisa Mwandamizi kutoka Idara ya Usimamizi wa Mifumo ya Fedha na TEHAMA wa Wizara ya Fedha, Bw. Charles Maganga, alipokuwa akitoa elimu ya matumizi ya namba ya malipo (Control Number) kwa malipo ya Serikali kwa wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar Es salaam (Sabasaba) yenye kaulimbiu ya “Maonesho ya Kibiashara ya Kimataifa Sabasaba, Fahari ya Tanzania” ambayo yameanza tarehe 28 Juni na kutarajiwa kuhitimishwa Julai 13 mwaka huu.