TIRA YATAKIWA KUDUMISHA VIWANGO VYA KIMATAIFA VYA UBORA WA HUDUMA
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, ameitaka Mamlaka hiyo kuhakikisha kuwa upatikanaji wa Cheti cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora ISO 9001:2015 unakuwa chachu ya kuimarisha uwajibikaji, ufanisi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi na wadau wa sekta ya bima nchini.
Ametoa msisitizo huo wakati wa hafla ya makabidhiano ya Cheti cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora ISO 9001:2015 kwa TIRA, iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka hiyo, Bima House, Njedengwa jijini Dodoma, ambapo alisema kupata cheti hicho si mwisho wa safari ya ubora, bali ni mwanzo wa hatua nyingine ya kuimarisha utendaji wa taasisi hiyo kwa kuzingatia viwango vinavyotambulika kimataifa.
