TANZANIA YATOA WITO WA KUONGEZA UWEKEZAJI KATIKA FEDHA ZA TABIANCHI.

Serikali ya Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuhamisha azma ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutoka katika mipango na ahadi kwenda kwenye uwekezaji na utekelezaji wa vitendo, ili kuhakikisha juhudi za kukabiliana na athari za tabianchi zinazaa matokeo yanayoonekana. Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula, wakati akifunga Mkutano wa Majadiliano Kuhusu Upatikanaji wa Fedha za Ufadhili wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi wa Mwaka 2026 (Tanzania Climate Finance Roundtable) chini ya kaulimbiu “Unlocking Climate Finance in the United Republic of Tanzania”, uliowakutanisha viongozi wa Serikali, washirika wa maendeleo, taasisi za fedha na sekta binafsi, uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.