TANZANIA YATOA NENO UKUBWA WA RIBA KIMATAIFA

Tanzania imeshiriki katika kikao cha Kwanza cha Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Ugharamiaji kwa Maendeleo Endelevu (Fouth International Conference on Financing for Deveoplopment - FfD4 kilichofanyika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia huku ikiutaka Umoja wa Mataifa (UN), kujadili upya na kupunguza riba za mikopo inayotolewa kwa nchi mbalimbali. Akizungumza katika kikao hicho mjini Addis Ababa nchini Ethiopia kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, alisema kutokana na shinikizo (pressure) la madeni inayozikabili nchi mbalimbali kama walivyosema baadhi ya wawakilishi wa nchi hizo, ni vyema Taasisi za Fedha za Kimataifa, zitoe mikopo yenye riba nafuu ili kuziwesha nchi zinazoomba mikopo ziweze kukuza uchumi na kufikia malengo ya maendeleo endelevu.