TANZANIA YALENGA MAPINDUZI YA UCHUMI KUPITIA UMEME NA NISHATI YA UHAKIKA
Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa inalenga kufanya umeme na nishati ya uhakika kuwa msingi wa mapinduzi ya uchumi yatakayochochea ukuaji wa viwanda, uwekezaji, ajira na maendeleo ya Taifa kuelekea mwaka 2050, huku ikilenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme hadi zaidi ya megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030/31.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, baada ya kuongoza Mkutano wa 35 wa Bodi ya Magavana wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (The African Capacity Building Foundation – ACBF), unaofanyika sambamba na Mkutano wa Afrika wa Taasisi za Tafiti na Majadiliano ya Sera (Africa Think Tank Summit – ATTS), mjini Cotonou, Jamhuri ya Benin.
