TANZANIA NA QATAR KUSHIRIKIANA KUKUZA SEKTA ZA FEDHA NA GESI ASILIA
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na kubadilishana uzoefu na nchi ya Qatar kukuza sekta ya fedha pamoja na utafiti, uchimbaji na uendelezaji wa gesi asilia ili sekta hizo ziweze kuchangia zaidi ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mhe. Balozi Omar amesema hayo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam, baada ya kupokea ujumbe maalumu kutoka nchi hiyo na kufanya mazungumzo na Balozi wa Qatar nchini Tanzania, Mhe. Fahad Rashid Al-Marekhi.
Alisema kuwa Qatar ina uzoefu mkubwa katika sekta ya utafutaji, uchimbaji na uendelezaji wa gesi asilia eneo ambalo Tanzania inaweza kujengewa uwezo zaidi.
