TANZANIA NA KENYA ZAAZIMIA KUIMARISHA ZAIDI UHUSIANO WA KIUCHUMI, KIBIASHARA NA KIDIPLOMASIA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Kenya zimeazimia kuendelea kushirikiana katika kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi (NTBs) vinavyoathiri mtiririko wa bidhaa, huduma na mitaji baina ya nchi hizo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha biashara na ushirikiano wa kiuchumi. Kauli hiyo ilitolewa tarehe 7 Oktoba, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, wakati akizungumza na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Catherine Kirumba Karemu, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.